Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Zaidi ya watu milioni 13 duniani hukumbwa na majanga ya asili, migogoro, na kuyumba kwa uchumi kila mwaka, huku zaidi ya milioni 83 wakilazimika kuhama makazi yao kutokana na athari za majanga hayo.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayojihusisha na Maafa (DINGONET), Ruger John Kahwa, ameeleza hayo leo Agosti 19,2025 Jijini hapa kwenye maadhimisho ya Siku ya Watoa Huduma za Misaada ya Kibinadamu Duniani, yaliyofanyika kitaifa kwa mara ya tatu, jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa Serikali kuingiza rasmi siku hii kwenye kalenda ya taifa, ili kuipa heshima inayostahili kwa mashujaa wa huduma za kibinadamu na kuongeza mshikamano wa kitaifa katika kukabiliana na majanga.
“Tanzania haiwezi kujitenga na changamoto hizi,hii ni siku muhimu ya kuenzi mashujaa wetu na ni wakati muafaka sasa serikali kuifanya kuwa sehemu ya kumbukumbu ya taifa letu,” amesema Kahwa.
Ameongeza kuwa tangu Januari hadi Juni 2025, watoa misaada kadhaa wamepoteza maisha wakitekeleza majukumu yao katika mazingira hatarishi, na hivyo kuna umuhimu wa kitaifa wa kutambua mchango huo kwa vitendo.
Katika tukio hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa tuzo ya heshima ya juu, kutambua mchango wake wa kipekee katika kushughulikia maafa, kuongoza kwa hekima wakati wa majanga, na kuhimiza utoaji wa misaada ya kibinadamu nchini.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa niaba ya Rais na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, ambaye pia amemwakilisha Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Lukuvi amesema kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha huduma za kibinadamu zinakuwa sehemu ya mfumo wa maendeleo endelevu nchini.
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kujiimarisha kupitia mipango maalum, ikiwemo kuanzisha “Situation Room” ya kitaifa, kwa ajili ya kufuatilia na kuratibu matukio ya majanga kwa wakati halisi, pamoja na kujenga miundombinu ya dharura, kugawa misaada ya chakula, makazi, huduma za afya, na msaada wa kisaikolojia kwa waathirika wa majanga.
Ametolea mfano kuwa, “Katika mafuriko makubwa ya mwaka 2024 yaliyotokea Kilosa, Kilombero, Rufiji na Kibiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau iliokoa maisha, kurejesha miundombinu na kuhakikisha wananchi wanarejea kwenye maisha ya kawaida,” amesema Lukuvi.
Amesisitiza kuwa Serikali imepokea kwa uzito ombi la DINGONET kutaka siku hii iwe rasmi kitaifa, na kuongeza kuwa hatua hiyo itafanyiwa kazi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Maafa.
Mbali na Rais Samia, tuzo ya pili imetolewa kwa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, na tuzo ya tatu ilimwendea Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa mchango wao mkubwa katika kuongoza juhudi za kukabiliana na maafa na kusaidia waathirika wa majanga nchini.
Taasisi zilizotunukiwa tuzo ya heshima ni pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (Tanzania Fire and Rescue Force)Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Wizara ya Ujenzi
,World Food Programme (WFP),UNICEF na Save the Children.
Nyingine ni World Vision International
Tanzania Red Cross Society (TRCS),Caritas Tanzania,RAPID Tanzania
,Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) na Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Uratibu wa Maafa
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Ummy Nderiananga, amesema kuwa watoa misaada ya kibinadamu ni mashujaa wa kweli wanaohitaji kuthaminiwa kwa dhati na jamii.
Amesema, “Utu na huruma havina mipaka,Kazi ya watoa misaada ni ya kipekee na ya kishujaa, ambayo Watanzania wanapaswa kushirikiana katika kuilinda na kuiendeleza,” amesema Ummy.
Amesema maadhimisho haya siyo tu ni kumbukumbu kwa waliopoteza maisha yao kazini, bali pia ni wito wa kitaifa kwa jamii nzima kushiriki kikamilifu katika kusaidia wenzao wakati wa majanga, ili kujenga taifa lenye ustahimilivu.
Maadhimisho ya mwaka huu ni ya tatu kufanyika nchini Tanzania, baada ya kuanza mwaka 2022 jijini Dar es Salaam, na kufuatiwa na ya mwaka 2024, pia jijini humo ambapo mwaka huu yamefanyika Jijini hapa yakiwa na kaulimbiu ya
“Kuimarisha Utoaji wa Huduma za Kibinadamu na Ustahimilivu Dhidi ya Majanga.”







Social Plugin