Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NJAMASII AVUTIA WAJUMBE WA CCM MPWAPWA KWENYE KINYANG'ANYIRO CHA UBUNGE



Na Barnabas Kisengi, Mpwapwa

Mbio za kuwania tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge wa Jimbo la Mpwapwa zimepamba moto baada ya kutangazwa kwa majina ya wagombea saba waliopitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho.

Kampeni za ndani za CCM, zilizoanza Julai 30 na zinatarajiwa kumalizika Agosti 3, 2025, zimekuwa na mvuto mkubwa huku kila mgombea akijipambanua kwa sera na mikakati ya maendeleo.

Miongoni mwa wagombea hao, Njamasii Chiwanga, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mazingira katika kampuni ya Lead Foundation (Kisiki Hai) wilayani Mpwapwa, ameonekana kung’ara kutokana na maono yake ya maendeleo na dhamira ya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.

Akihutubia wajumbe wa CCM katika kata mbalimbali, Chiwanga aliahidi kushirikisha jamii katika maamuzi ya maendeleo na kuhakikisha utekelezaji wa ilani ya chama hicho kwa vitendo.

“Nitahakikisha utekelezaji wa ilani ya CCM unatekelezwa ipasavyo, ikiwemo kutoa mikopo kwa wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu. Dhamira yangu ni kuwatumikia wananchi kwa moyo wa uwajibikaji na ushirikishwaji,” alisema Chiwanga.

Chiwanga, ambaye ni mtoto wa Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglican na baba yake aliyehudumu kama Waziri wa Elimu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, amejipambanua kama kiongozi mwenye uzoefu na maono mapana ya maendeleo.

Uchaguzi wa kura za maoni kwa ajili ya kumpata mgombea wa CCM katika Jimbo la Mpwapwa unatarajiwa kufanyika kesho, Agosti 4, 2025, ambapo mwanachama mmoja ataibuka mshindi na kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com