Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDUMBARO ATOA WITO WA UMOJA SONGEA MJINI: "TUVUNJE MAKUNDI, TUTAFUTE USHINDI WA PAMOJA"


Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma

Mgombea wa nafasi ya ubunge katika Jimbo la Songea Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Damas Ndumbaro, ametoa wito wa mshikamano na kuvunjwa kwa makundi ndani ya chama, amesisitiza kuwa umoja ndiyo silaha ya ushindi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama kuwania nafasi hiyo, Dkt. Ndumbaro amewaomba wanachama kuwa kitu kimoja na kuacha migawanyiko isiyo na tija.

Dkt. Ndumbaro amesema kuwa kuanzia sasa ni muhimu kwa wanachama wote kuachana na makundi na kushikamana kwa pamoja, amesisitiza kuwa kutomuunga mkono mgombea atakayeteuliwa na chama ni sawa na usaliti.

Amesema kuwa mshikamano wa kweli ni msingi wa ushindi, na kwamba kila mwanachama ana wajibu wa kulinda umoja wa chama kwa manufaa ya wananchi wa Songea mjini na Tanzania kwa ujumla.

Katika kuonesha mfano wa umoja, Dkt. Ndumbaro ametumia jukwaa hilo kuwatambulisha hadharani baadhi ya watia nia waliogombea nafasi hiyo ya ubunge kupitia chama hicho, jambo lililopokelewa kwa heshima na shangwe kutoka kwa wanachama waliokuwepo.

Amesema hatua hiyo ni kielelezo cha demokrasia na mshikamano unaojengwa ndani ya chama.

Wito wa Dkt. Ndumbaro umeonekana kuwagusa wanachama na wafuasi wa chama hicho, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo mshikamano, heshima na umoja vinahitajika zaidi ili kuhakikisha ushindi wa chama katika Jimbo la Songea Mjini.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com