Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NCCR MAGEUZI YATEUA WAGOMBEA NA KUPITISHA ILANI YA UCHAGUZI 2025



Na Dotto Kwilasa, Dodoma


Ikiwa imesalia siku moja kabla ya kufungwa kwa zoezi la uchukuaji fomu za uteuzi kwa wagombea wa Urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha NCCR Mageuzi imefanya kikao maalum leo Agosti 14, 2025 jijini Dodoma, kikiwa na ajenda kuu ya maandalizi ya uchaguzi.

Katika kikao hicho, wajumbe wote 58 waliopiga kura wamemteua Balozi Dkt. Evaline Wilbard Munisi kuwa mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiungana na  Haji Ambar Khamis ambaye tayari aliteuliwa kuwa mgombea Urais wa Jamhuri katika kikao kilichopita. 

Vilevile, Leila Rajabu Khamis ameteuliwa kuwa mgombea Urais wa Zanzibar baada ya kupata kura 57 kati ya 58 za wajumbe waliohudhuria.

Kikao hicho pia kimeidhinisha Ilani ya Uchaguzi 2025/2030 yenye vipaumbele 11, ikiwemo sekta ya afya, usawa wa kijinsia na makundi maalum, mifugo, madini, maliasili na utalii, usalama wa taifa, pamoja na kurejesha maadili ya kitaifa.
 Kipaumbele cha maadili na uadilifu kimepigiwa chapuo la kipekee na viongozi wa chama hicho.

Akizungumza baada ya kikao,Mwenyekiti wa chama hicho Hajji Ambar Khamis amesema  kuwa uteuzi wa wagombea hao ni matokeo ya majadiliano ya kina na makubaliano ya pamoja.
 Viongozi hao wamesisitiza kuwa sera ya chama inalenga utu na maendeleo endelevu, badala ya kushindana kwa hoja ya kuiondoa CCM madarakani kama msingi pekee.

“Niwatoe hofu ndugu zangu, kama tulivyosema kwenye azimio letu, lazima tushinde,” amesema .

Aidha amebainisha kuwa NCCR Mageuzi imesimamisha wagombea ubunge katika majimbo yote 162 na kurejeshaongeza kuwa chama hakipokei ruzuku ya Serikali bali hutegemea michango ya wanachama na wananchi.

Ameeleza kuwa licha ya chama hicho kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kuusaka urais haimaanishi kwamba chama kilichopo madarakani (CCM) hakijafanya maendeleo yoyote. 

Amesisitiza, "Tunajua CCM imefanya maendeo makubwa tu lakini na Sisi tunataka tufike mbali zaidi hivyo tutakapoingia madarakani tutaanzia walipoishia wenzetu, " Ameeleza

 Kwa upande wake, Sisty Nyahoza, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa aliyemwakilisha Msajili wa Vyama, aliipongeza NCCR Mageuzi kwa kufanya kikao chake cha kikatiba kwa utulivu na kuzingatia misingi ya demokrasia. 

Ametoa rai kwa viongozi na wanachama wa chama hicho kuendesha kampeni kwa kuzingatia katiba, sheria na miongozo husika, hasa kuelekea kuanza kwa kampeni rasmi Agosti 28, 2025.

Ameongeza kuwa, licha ya baadhi ya vyama kutoshiriki uchaguzi kwa hiari yao, NCCR Mageuzi imeonyesha dhamira ya dhati ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia na kutumia haki yake ya kikatiba.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com