Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIJIJI CHA NGWALA CHAJIFUNZA SIRI YA MAFANIKIO MUNDINDI

Ofisi ya halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe ambapo wageni kutoka Ngwala-Songwe wakiwa katika picha ya pamoja na wenyeji wao wa kijiji cha Mundindi Wilayani humo walipotembelea kwa lengo la kujifunza matumizi bora ya fidia

Na Mwandishi Wetu Malunde 1 Blog Ludewa- Njombe

Kijiji cha Mundindi, wilayani Ludewa, kimeendelea kuwa mfano wa matumizi bora ya fidia baada ya kupokea ugeni wa viongozi 30 kutoka Kijiji cha Ngwala, Wilaya ya Songwe. 

Ugeni huo ulipokelewa rasmi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Ndg. Sunday Deogratias, ambaye ameeleza kuwa ziara hiyo ni ushahidi wa jinsi maendeleo yanaweza kuchochewa endapo rasilimali zinatumika kwa uwazi na mipango endelevu. 

Ndg. Deogratias, ambaye ni mchumi kitaaluma na mwenye uzoefu mpana katika usimamizi wa fedha za umma, amesema kuwa maendeleo ya kweli huanza na maamuzi sahihi ya viongozi wa ngazi za chini hadi juu.

Ziara hiyo imejikita katika kujifunza kutoka mafanikio ya Kijiji cha Mundindi ambacho kilipokea fidia ya zaidi ya shilingi milioni 460 kutoka Mradi wa Liganga. 

Kupitia usimamizi madhubuti wa Halmashauri kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji, fedha hizo zilitumika kununua bima za afya kwa wananchi wote, hatua iliyosaidia kuondoa mzigo wa gharama kubwa za matibabu na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya. 

Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Twilumba Lihweuli, amesisitiza kuwa hali ya afya ya wananchi wa Mundindi imeimarika, huku matumizi ya tiba za asili yakipungua kwa kiasi kikubwa kutokana na upatikanaji wa huduma za kisasa.

Katika hatua ya kuongeza tija ya fidia hiyo, Kijiji cha Mundindi kimenunua dhamana (bond) ya shilingi milioni 400 kupitia Benki ya CRDB, ikiwa ni mkakati wa kulinda thamani ya fedha na kujihakikishia mapato endelevu kwa ajili ya miradi ya kijiji kwa miaka ijayo. 

Meneja wa Kanda wa CRDB, Bi. Domina Mwita, ambaye benki yake ilidhamini ziara hiyo, amepongeza uongozi wa kijiji kwa kuwa na maono ya muda mrefu katika usimamizi wa rasilimali. 

Wageni kutoka Ngwala wamepata fursa ya kutembelea zahanati, kukutana na uongozi wa kijiji, na kujifunza namna uwazi na ushirikishwaji wa jamii ulivyosaidia kufanikisha mpango huo.

Wananchi wa Mundindi, akiwemo Flowini Mgaya na Clementina Mkinga, wamewashirikisha wageni uzoefu wao wa kunufaika na bima za afya, wakisema sasa wana uhakika wa matibabu bila wasiwasi wa gharama. 

Wajumbe kutoka Ngwala wameondoka wakiwa na hamasa kubwa ya kuiga mfano huo wa mafanikio, wakiahidi kupeleka nyumbani walichojifunza ili kuhakikisha fidia yoyote wanayopokea itumike kwa manufaa ya jamii yote.Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe Ndugu Sunday Deogratias akizungumza na wajumbe kutoka Ngwala-Songwe 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com