Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake kwa kuandika historia mpya katika sekta ya madini nchini, baada ya kuanza rasmi kwa ujenzi wa maabara ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini inayojengwa katika eneo la Kizota, Dodoma.
Katika tukio hilo la kihistoria lililofanyika Agosti 25, 2025 Jijini Dodoma Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara hiyo ambayo inatarajiwa kuwa kubwa zaidi na ya kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Maabara hiyo inatarajiwa kugharimu Shilingi Bilioni 14.3 na kukamilika ndani ya kipindi cha siku 690.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Mavunde amesema
kuwa GST imekuwa taasisi ya kimkakati kwa maendeleo ya sekta ya madini, na ujenzi wa maabara hiyo unaonesha dhamira ya serikali ya kuwekeza katika utafiti wa kisayansi kama msingi wa uchimbaji wa kisasa wa madini.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, bajeti ya sekta ya madini imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, jambo linaloashiria dhamira ya kweli ya mageuzi.
“Katika historia ya madini, bajeti imekuwa ikigota kwenye hatua fulani. Lakini kwa sasa, tunaona ongezeko la rasilimali kwa ajili ya utafiti kupitia GST – taasisi ambayo ni moyo wa sekta ya madini nchini.
" Hatuwezi kuendeleza madini bila utafiti wa kisayansi,tunapaswa kuwekeza zaidi kwenye utafiti ” amesema Mavunde
Amebainisha kuwa kupitia maabara hiyo, serikali inalenga kuwasaidia wachimbaji wadogo na wakubwa kupata taarifa sahihi za sampuli za madini, hali itakayowaondoa katika uchimbaji wa kubahatisha na hivyo kuongeza tija.
Aidha, ametangaza kuwa Rais ameridhia mchakato wa ununuzi wa helikopta maalum kwa ajili ya kufanya tafiti za awali za kijiolojia, hatua itakayoiweka Tanzania katika nafasi ya juu ya kitaalam barani Afrika.
Waziri Mavunde pia amesema kuwa ndoto yake ni kuiona GST ikijitanua na kuwa taasisi kubwa barani Afrika, yenye uwezo wa kufanya tafiti za kina na kutoa huduma za kisasa kwa Afrika nzima.
Amesisitiza kuwa Tanzania sasa imejielekeza kwenye utafiti kama njia kuu ya kuhakikisha sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye pato la taifa.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST, Dkt. Notka Huruma Batenze, amesema kuwa miaka 100 ya taasisi hiyo imejaa historia ya mafanikio makubwa, lakini sasa wanajielekeza kwenye karne ya pili kwa nguvu mpya na dira ya kisasa.
Amesema maabara hiyo itaongeza uwezo wa utoaji wa huduma bora za kimaabara kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu, na hivyo kusaidia taifa kupata taarifa za kisayansi kwa maamuzi ya uwekezaji.
Ameeleza kuwa maabara hiyo ni nyenzo muhimu katika kusaidia nchi kufikia uchumi wa viwanda kupitia matumizi bora ya rasilimali madini.






Social Plugin