Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DODOMA KUFUNGUA MILANGO YA AJIRA KUPITIA KIWANDA CHA ZHONG ZHOU



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Wananchi wa Kata ya Zanka, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wanasema ndoto zao za muda mrefu za maendeleo zimeanza kuota mizizi, kufuatia uzinduzi wa kiwanda kikubwa cha kusindika na kuyeyusha madini ya Nikeli na Shaba, kinachomilikiwa na kampuni ya Zhong Zhou.

Kiwanda hicho, ambacho kinatarajiwa kutoa zaidi ya ajira 300 za moja kwa moja, kimeibua matumaini mapya kwa jamii inayozunguka, wakiwemo wachimbaji wadogo, vijana, na wanawake wajasiriamali. 

Fursa hizi mpya si tu itaongeza kipato, bali pia zitachochea ukuaji wa biashara ndogo ndogo na uboreshaji wa huduma za kijamii katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi leo, Agosti 26, 2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza kwa vitendo sera ya kuongeza thamani ya madini kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi.

 “Tumeacha kusafirisha udongo wala mawe,Sasa tunachakata madini yetu hapa nchini na kuongeza thamani kwa faida ya taifa na wananchi wake,” amesisitiza Mavunde huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kiwanda hicho ni sehemu ya mkakati  wa Serikali wa kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kwa kutoa ajira, kuendeleza ujuzi wa ndani na kuchangia mapato ya taifa kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Mavunde amesema, Viwanda nane vya uchakataji wa dhahabu vinafanya kazi nchini, na viwanda vingine vitano vinaendelea kujengwa mkoani Dodoma kwa lengo la kuongeza thamani ya madini kama shaba, nikeli, na mengineyo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt.Abdulrahman Mwanga amesema hatua hiyo ni ushahidi wa mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyoandaliwa na serikali kwa kusimamia sheria na sera za sekta hiyo kwa weledi na ufanisi.

“Zamani ilikuwa vigumu kuona viwanda kama hivi hapa nchini,lakini sasa tunashuhudia mageuzi makubwa. Wachimbaji wadogo wanapaswa kutumia fursa hii kujiendeleza zaidi,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wawekezaji wankiwanda hicho Zhong Zhou kushirikiana kwa karibu na jamii inayowazunguka, si tu kwa kutoa ajira, bali pia katika miradi ya kijamii kama afya, elimu na miundombinu.

Kutoka na hayo baadhi ya Wananchi nao wameeleza matumaini yao kuwa uwepo wa kiwanda hicho utakuwa chachu ya kuimarika kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja, huku vijana wakipata nafasi ya kujifunza teknolojia mpya za uchakataji madini.

John Mabegele amesema hatua hiyo itawasaidia kujiimarisha kiuchumi na kuelezea kuwa wao kama wanufaika wakubwa watasimama bega kwa bega kushirikiana na serikali  katika utekelezaji wa sera ya "Madini ni Maisha na Utajiri," kwa kuamini kuwa sekta hiyo ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com