Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma imeanza ujenzi wa daraja la Mitomoni katika Mto Ruvuma lenye urefu wa mita 45, litakalounganisha Wilaya ya Nyasa na Songea.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Saleh Juma, amesema ujenzi wa daraja hilo ambalo hadi sasa umefikia asilimia 65, unagharimu Shilingi bilioni 9.295 zilizotolewa na Benki ya Dunia, na unatekelezwa na Kampuni ya Kitanzania ya Ovans Construction Ltd. Ameeleza kuwa daraja hilo litaunganisha barabara ya Unyoni–Mpapa–Lipalamba–Mkenda na barabara ya Likuyufusi–Mkenda, na linatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mhandisi Saleh, daraja hilo litatatua changamoto kubwa ya mawasiliano kati ya Wilaya ya Nyasa, Songea na nchi jirani ya Msumbiji, hasa wakati wa masika ambapo mto Ruvuma hujaa maji na kusababisha wananchi wa vijiji vya Mitomoni na Mkalawa kushindwa kuvuka. Ameongeza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii, kuimarisha uchumi na usalama wa maeneo hayo na kuchochea maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Pius Gwegendao, amesema watahakikisha mkandarasi anatekeleza ujenzi kwa viwango vilivyopangwa.
Naye Mwakilishi wa Mkandarasi, Mhandisi Emanuel Bilai, amesema mradi huo unahusisha pia ujenzi wa barabara unganishi ya lami yenye urefu wa kilomita 8, na daraja hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kupitisha magari mawili kwa wakati mmoja pamoja na njia za watembea kwa miguu pande zote mbili.
Ameeleza kuwa ujenzi wa nguzo moja umekamilika na ujenzi wa nguzo ya pili unaendelea sambamba na kuta ya katikati ya maji.Wananchi wa vijiji vya Mitomoni na Mkalawa wameipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi wa daraja hilo, wakieleza kuwa litamaliza mateso ya kutumia mitumbwi kuvuka mto huo, hali ambayo imewasababisha kupoteza maisha ya ndugu zao hususan nyakati za mvua nyingi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkalawa, Zuber Mohamed, na wa Mitomoni, Ali Mpaiche, wameeleza kuwa daraja hilo litaokoa maisha, kurahisisha elimu kwa watoto, kusaidia akina mama wajawazito kupata huduma bora kwa wakati na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Wameiomba Serikali kuhakikisha mkandarasi anakamilisha kazi hiyo kwa wakati kama ilivyopangwa.Muonekano wa mto Ruvuma unaotenganisha Wilaya ya Nyasa na Songea Mkoani Ruvuma
Social Plugin