
Anna Tenga, Mkurugenzi Mkazi WaterAid Tanzania
Na Deogratius Temba – Hanang, Manyara
WaterAid Tanzania kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wameendesha mafunzo kuhusu ujumuishaji wa masuala ya usawa wa kijinsia (GESI) katika sekta ya maji, usafi wa mazingira na usafi wa mikono (WASH) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’.
Mafunzo hayo yamewakutanisha watumishi wa umma kutoka idara mbalimbali za Halmashauri ya Hanang’, Ofisi ya Mipango ya Mkoa wa Manyara na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Rehema Msumi, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango wa Halmashauri ya Hanang’, alisema:
“Tunachowahakikishia ni kwamba yale tuliyojifunza hapa tutayatekeleza. Mwisho wa siku tutakutana tena kwa ajili ya mrejesho kuona tulivyotekeleza. Tutahakikisha bajeti zetu zinaakisi usawa wa kijinsia hasa kwenye eneo la WASH, na mipango hii itatekelezwa kwa matokeo chanya.”
Kwa upande wake, Anna Tenga, Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid Tanzania, aliwashukuru washiriki na wadau wote waliowezesha mafunzo hayo:
“Tunawashukuru sana wadau wetu na hasa watumishi wa umma waliokubali kushiriki mafunzo haya na kutumia muda wao kujifunza, hususan maafisa bajeti. Ni matarajio yetu ujuzi huu utasaidia kuhakikisha bajeti inakuwa jumuishi na inagusa mahitaji ya wanawake, wanaume, wasichana, wavulana pamoja na watu wenye ulemavu katika huduma za WASH.”
Naye Elias Ermias, Mshauri wa GESI wa WaterAid Kanda ya Afrika Mashariki na mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pamoja:
“Mafunzo haya hayapo kwa Hanang’ pekee. Tunataka yawe chachu ya kuigwa na halmashauri nyingine. Tunapenda Hanang’ iwe mfano wa mafanikio, jitihada za WaterAid zikisaidia kuboresha maisha ya kila mtu kupitia huduma bora za WASH.
Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ambakisye Mhiche, Afisa Afya na Mazingira, alisema: “Tumejifunza mambo muhimu sana. Tunatambua mchango wa wadau wetu na tunaahidi kupeleka elimu hii nje ya Hanang’. Mafunzo haya yataboresha maisha ya wananchi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika mipango ya WASH.”
Kwa ujumla, mafunzo haya yamelenga kuhakikisha sera, mipango na bajeti za Halmashauri zinakuwa jumuishi. TGNP imechangia pakubwa katika kuwajengea uwezo maafisa mipango na bajeti ili kuhakikisha utekelezaji wa bajeti zenye mtazamo wa kijinsia.






Social Plugin