
Na Goodluck Mwihava - WANMM
Wachezaji wa Timu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wamehimizwa kuzingatia nidhamu, mshikamano na kujituma kwa bidii ili kuleta ushindi, sambamba na kuitangaza Wizara na Serikali wakati wa mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI 2025) yatakayofanyika jijini Mwanza kuanzia Septemba 1 hadi 16, 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi, Bw. Deogratious Kalimenze, aliwahimiza wanamichezo hao kuwa ushindi hautokani na uwezo wa mtu mmoja bali mshikamano,Kujituma na nidhamu ya pamoja.
“Kumbukeni mnaibeba Wizara yetu. Nidhamu, mshikamano na kupambana kwa bidii ndiyo silaha ya ushindi. Wizara iko bega kwa bega nanyi, hivyo jitahidini kushiriki kwa juhudi na kurejea na ushindi ,” alisema Kalimenze.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bi. Prisca B. Lwangili, aliwatakia kila la heri wachezaji hao na kuwataka kupambana kwa ari na ujasiri ili kuipa heshima Wizara.
Aidha, Katibu wa Klabu, Bw. Adam Komba, aliwahakikishia viongozi na wadau wa michezo kuwa maandalizi ya timu yako imara, na kwamba wachezaji wako tayari kushindana katika michezo yote kwa lengo la kurejea na ushindi.




Social Plugin