Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JEREMIAH JILILI AONYESHA UKOMAVU WA KISIASA, AAPA KUBAKI MWAMINIFU KWA CCM

 

Licha ya jina lake kutorudishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge Jimbo la Solwa, mwanasiasa chipukizi Jeremiah Jilili ameonyesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa kwa kuendelea kusimama na chama chake bila kuyumba.

Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mitandao ya kijamii, Jilili amesema amepokea kwa heshima na unyenyekevu maamuzi ya chama, akieleza kuwa anaamini si kila wakati matamanio na mipango ya kibinadamu huendana na makusudi ya Mwenyezi Mungu.

"Nimepokea uamuzi huu wa kutoteuliwa kwa unyenyekevu na moyo wa ustahimilivu. Nimesimama imara nikiwa mwanachama mwaminifu wa chama changu, nikiamini kuwa maslahi ya chama ni ya msingi kuliko yangu binafsi," ameandika Jilili.

Jilili ameahidi kuendelea kushirikiana na kuunga mkono juhudi za chama chake kwa moyo wote, akisisitiza kuwa mshikamano wa chama ndio msingi wa ushindi katika siasa.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema msimamo huu wa Jilili unaonesha picha ya kiongozi kijana mwenye nidhamu, aliye tayari kujifunza na kusubiri wakati wake. Hatua yake imetajwa kama fundisho kwa wanasiasa wengine, ikionesha kwamba uaminifu kwa chama na uvumilivu ni silaha muhimu za kisiasa.

Hii ni ishara ya ujasiri na uadilifu wa kisiasa. Jilili amejijengea heshima kubwa kwa kukubali maamuzi ya chama bila malalamiko, jambo linalomfanya awe na mustakabali mzuri kisiasa,” amesema mchambuzi mmoja.

Kwa msimamo huu, Jilili ameibuka sio tu mwanachama wa CCM, bali pia kielelezo cha siasa za kistaarabu na mshikamano wa chama.

WALIOTEULIWA KUGOMBEA UBUNGE SOLWA

Katika mchakato wa ndani ya chama, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imempitisha Ahmed Ally Salum kugombea tena nafasi ya ubunge katika Jimbo la Solwa, mkoani Shinyanga. Sambamba na Ahmed, walioteuliwa kushiriki katika mchujo wa awali ni Sosthenes Julius Katwa, Selemani Emmanuel Choka, Zinguji Mayala Machwele, Leonard Nduta Lukanya, Alphistone Michael Bushi na Costantine Joseph Budaga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com