
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mtandao wa Wanablogu Tanzania (Tanzania Bloggers Network - TBN) umevitaka vyama vya siasa, wagombea na wananchi kudumisha amani na kufuata sheria katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu unaoendelea nchini.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa Agosti 28, 2025 na Mwenyekiti wake, Beda Msimbie, TBN imesisitiza kuwa utunzaji wa amani ni jukumu la kila mmoja na kuhimiza kampeni zifanyike kwa ustaarabu bila kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.
“Tunaomba vyama vyote vya siasa vitumie kipindi hiki kueleza ilani zao kwa wananchi kwa njia ya ustaarabu na bila kuhatarisha amani tuliyonayo. Ni wajibu wa kila chama na kila mgombea kuhakikisha kampeni zinabaki kuwa chachu ya maendeleo na siyo chanzo cha migawanyiko,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, TBN imewahimiza wanachama wake zaidi ya 200 kutumia majukwaa ya kidijitali kusambaza habari sahihi na za uwajibikaji ili kusaidia wananchi kuelewa ilani za vyama na kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.
Mtandao huo pia umeihakikishia Serikali kuwa uko tayari kushirikiana nayo katika kulinda utulivu wa nchi na kupambana na taarifa za upotoshaji zinazoweza kuhatarisha amani. Umewataka wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kusambaza habari za uchochezi au zisizo na ukweli.
Kwa mujibu wa TBN, blogu na mitandao ya kijamii vina nafasi muhimu ya kuimarisha mshikamano na demokrasia, hivyo wadau wote wametakiwa kutumia majukwaa hayo kuilinda Tanzania dhidi ya siasa potofu.
Social Plugin