Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linamshikilia mwanamke aitwaye Wende Luchagula kwa tuhuma za mauaji ya watoto watatu, wakiwemo mapacha wawili wa mke mwenzie.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea tarehe 12 Julai 2025 katika kijiji cha Milonji, kata ya Lusewa, Wilaya ya Namtumbo, ambapo inadaiwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 25 Julai 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco G. Chilya, amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alitekeleza mauaji hayo majira ya saa nane mchana.
Watoto waliouawa ni Kulwa Lutelemula Samweli na Doto Lutelemula Samweli (mapacha wenye umri wa miezi 8) pamoja na Lugola Lutelemula mwenye umri wa miaka 6, wote wakazi wa kijiji cha Milonji.
Kamanda Chillya amesema Jeshi la Polisi limechukua hatua stahiki kuhakikisha mtuhumiwa anafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Ameeleza kuwa tukio hilo limelishtua na kulihuzunisha taifa, hasa kutokana na kuhusisha vifo vya watoto wadogo wasio na hatia.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limetoa wito kwa wanandoa wote walio katika ndoa za wake zaidi ya mmoja kuwa wavumilivu na kujiepusha na wivu wa kupindukia.
Imesisitizwa kuwa migogoro ya kindoa inaweza kutatuliwa kwa njia ya amani kwa kushirikisha viongozi wa dini, wazee wa familia au viongozi wa jamii.
Jeshi hilo pia limetoa rai kwa jamii kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa mapema pale panapojitokeza dalili za migogoro au vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani, ili kuzuia madhara makubwa kama haya yasijirudie.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Mkoani Ruvuma SACP Marco G Chilya akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mauaji yaliyotokea katika kijiji cha Milonji kata ya lusewa wilayani Namtumbo

Social Plugin