Na Dotto Kwilasa, Mtumba - Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu William Lukuvi, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutimiza kikamilifu ndoto ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhamishia ofisi zote za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba.
Akizungumza Julai 23, 2025, wakati wa ziara maalum ya kukagua utekelezaji wa maagizo ya Rais kuhusu ujenzi wa majengo ya awamu ya pili, Lukuvi amesema Wizara hiyo imeonyesha mfano bora wa utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa vitendo.
“Majengo haya yamejengwa kwa awamu mbili awamu ya kwanza ni wakati wa Hayati Dkt. John Magufuli, na awamu ya pili ni chini ya Rais Samia ambapo ujenzi wake ni wa kisasa zaidi na wa ghorofa. Nawapongezeni kwa kutimiza agizo la Rais na kuonyesha uzalendo wa kweli. Mmekuwa wa kwanza sio tu kukamilisha jengo bali pia kuhamia. Hongereni sana,” amesema Mhe. Lukuvi.
Aidha, Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa kutumia rasilimali za ndani katika ujenzi na uendeshaji wa ofisi hizo, akipongeza hatua ya wizara kutumia samani zilizotengenezwa kwa mbao za hapa nchini. “Nyinyi ni wasimamizi wa misitu nchini, mmeonyesha njia kwa kutumia mbao kutoka ndani ya nchi. Huu ni mfano wa kuigwa,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, amesema kukamilika kwa jengo hilo ni kielelezo cha dhamira ya Rais Samia ya kuboresha huduma za umma na kuongeza ufanisi katika sekta ya maliasili na utalii.
Ameeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 20, na sasa limekamilika kwa viwango vya kimataifa likiwa na uwezo wa kuchukua idadi kubwa ya watumishi huku likiwa na miundombinu rafiki kwa mazingira na watu wenye uhitaji maalum.
Dkt. Abbas ameongeza kuwa kuhamia Mtumba si tu kunaleta ufanisi katika utendaji kazi bali pia kunatoa nafasi ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi katika muktadha wa Serikali kuhamia rasmi Dodoma.
Mabadiliko haya makubwa yanatajwa pia kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa maeneo ya jirani na Mtumba, kutokana na uwepo wa watumishi wa Serikali, biashara, na huduma mbalimbali zinazochipuka kwa kasi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), majengo ya awamu ya pili ya wizara mbalimbali yanatarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwaka 2025, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuimarisha Mji wa Serikali.
Wizara ya Maliasili na Utalii sasa imejihakikishia historia ya kuwa ya kwanza kukamilisha ujenzi na kuhamia rasmi Mtumba, hatua inayotajwa kuwa kielelezo cha nidhamu, utekelezaji wa haraka wa maelekezo ya Serikali na uzalendo wa kweli kwa viongozi wake.






Social Plugin