
Mchakato wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 umeibua majina kadhaa ya wanachama waliotangaza nia katika Jimbo la Shinyanga Mjini.
Taarifa kutoka ndani ya CCM, mazungumzo ya wanachama, mitandao ya kijamii na mijadala isiyo rasmi, zimeendelea kuwazungumzia zaidi baadhi ya watia nia wanaoonekana kuwa na harakati zilizoibua mijadala ndani na nje ya chama.
Baadhi ya majina ya watia nia yamekuwa yakitajwa mara kwa mara na kujadiliwa zaidi kutokana na nafasi zao za sasa au historia yao ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, hasa miongoni mwa wanachama na wachambuzi wa siasa za ndani ya CCM.
1. Patrobas Katambi
Patrobas Katambi ni Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, na pia Mbunge anayemaliza muda wake katika Jimbo la Shinyanga Mjini.
Ameshachukua na kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama. Katika mazungumzo ya wanachama na kwenye vikao visivyo rasmi, jina lake limekuwa likitajwa kwa kuwa tayari alishawahi kuliongoza jimbo hilo kwa miaka mitano.
Kauli yake kuwa "Bado nina nguvu ya kuwatumikia" imeendelea kujadiliwa kama ishara ya kutaka kuendeleza kile kilichoanzishwa.
2. Stephen Julius Masele
Stephen Masele ni mwanasiasa aliyewahi kulitumikia jimbo la Shinyanga Mjini kwa miaka kumi (2010–2020). Akiwa pia amewahi kushika nafasi ya Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika na Naibu Waziri, jina lake limeanza kusikika zaidi baada ya kuchukua fomu ya CCM.
Kauli zake kuhusu kurejesha furaha na mshikamano kwa wananchi zimekuwa sehemu ya mijadala ya kisiasa ndani ya mji wa Shinyanga. Wanachama mbalimbali wamekuwa wakimjadili kutokana na historia yake ya kisiasa na nafasi alizowahi kushika serikalini na kimataifa.
3. Mhandisi James Jumbe Wiswa
Mhandisi Jumbe ni kada wa muda mrefu wa CCM na mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya. Taarifa zake za kuchukua na kurejesha fomu ziliripotiwa kwa utulivu na nidhamu, jambo lililovutia baadhi ya wanachama waliodai kuwa ni mtu wa mchakato na mwenye mtazamo wa kimfumo.
Katika baadhi ya mijadala ya ndani ya chama, Jumbe ameendelea kusemwa kutokana na ushiriki wake wa karibu na shughuli za kisiasa za wilaya, kijamii pamoja na kauli zake zinazozingatia maadili ya chama.
4. Fahad Gulamhafiz Mukadam
Fahad Gulamhafiz Mukadam anatambulika kwa asili yake ya kisiasa akiwa mtoto wa mwanasiasa mkongwe na Meya mstaafu wa Manispaa ya Shinyanga, Mzee Gulamhafiz Mukadam.
Mbali na msingi huo wa kifamilia, Fahad ni mwekezaji, kiongozi wa biashara, na mtaalamu wa masoko na teknolojia. Ameanzisha na kuongoza kampuni kadhaa zikiwemo Octopus International, Koikoi Pro na Brands & Stories Ltd, sambamba na kutoa ushauri wa kimkakati kwa kampuni binafsi.
Anaelezwa kuwa na uzoefu katika masoko ya kidijitali, tafiti za soko, na ushawishi kupitia mitandao ya kijamii.
Jina lake limeendelea kusemwa zaidi baada ya kuchukua fomu ya CCM, na baadhi ya wanachama wanamtazama kama sura mpya inayobeba nguvu ya kizazi kipya chenye maono ya kisasa na weledi wa kiuchumi.
5. Gilitu Makula
Gilitu Makula ni mfanyabiashara anayetambulika ndani ya mji wa Shinyanga na ni miongoni mwa makada wa CCM waliotangaza nia ya kugombea ubunge kwa kuchukua fomu katika mchakato wa ndani ya chama. Ingawa hana historia ya moja kwa moja ya kushika nafasi za kisiasa au serikali, jina lake limeendelea kutajwa mara kwa mara katika mijadala ya ndani ya chama, hasa kutokana na nafasi yake katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Wapo wanaomtazama kama sura mpya inayotoka nje ya mfumo wa kisiasa wa kawaida, lakini anayejijengea ushawishi kupitia kazi zake katika jamii. Uwepo wake umehusishwa na sauti za baadhi ya wanachama wanaotamani kuona sura mbadala kutoka sekta binafsi, wakiamini kuwa uzoefu wa usimamizi na uendeshaji wa biashara unaweza kuwa mtaji wa kiuongozi.
Katika vikao visivyo rasmi, jina la Gilitu limekuwa likitajwa miongoni mwa watia nia wanaoibua mijadala kuhusu nafasi ya wafanyabiashara na sekta binafsi katika michakato ya kisiasa, jambo linalowafanya baadhi ya wanachama kumjadili kwa mtazamo tofauti na wa kawaida.
Majina ya Patrobas Katambi, Stephen Masele, James Jumbe Wiswa, Fahad Mukadam na Gilitu Makula yameendelea kuzungumzwa kwa kiwango kikubwa katika muktadha wa mchakato wa ndani ya CCM Jimbo la Shinyanga Mjini.
Hili linaonyesha namna majina hayo yalivyochochea mijadala ya kisiasa ndani ya chama na miongoni mwa wananchi.
Hata hivyo, uamuzi wa mwisho utatokana na mchakato wa chama kwa mujibu wa taratibu na vikao halali vya kikatiba kwani makada wengi wa CCM wamejitokeza katika kinyang'anyiro cha kuwania ubunge katika jimbo la Shinyanga Mjini.
Social Plugin