Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI KISHAPU WAUNGANA KUFANYA USAFI, DAMPO LA KISASA LAJA


Afisa Mazingira wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Charles Kanwakabo akizungumza baada ya zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi Julai 26,2025

Na Sumai Salum - Kishapu

Katika kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa safi na salama kwa afya ya jamii, Afisa Mazingira wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Charles Kanwakabo, amesema kuwa desturi ya kufanya usafi wa maeneo yote ya shughuli za kijamii imeendelea kuungwa mkono kwa kiwango cha kuridhisha.

Amesema kuwa mwitikio wa wananchi, wanafunzi na viongozi katika zoezi la usafi lililofanyika Julai 26, 2025 ni wa kuvutia, na hadi sasa hali ya usafi imefikia kiwango cha asilimia 85 hali inayoonesha mwamko mpya wa utunzaji wa mazingira miongoni mwa jamii.

"Tunashukuru wananchi, viongozi na wanafunzi wa Kishapu Sekondari kwa kushiriki kikamilifu licha ya mafanikio haya, tunasisitiza kuwa usafi usiwe zoezi la kila mwisho wa mwezi pekee, bali uwe sehemu ya maisha ya kila siku ya wananchi,” amesema Kanwakabo.

Aidha, ametoa rai kwa wakazi wa Kishapu kuacha kusubiria maagizo ya viongozi ili kushiriki usafi, bali wajenge tabia ya kudumu ya kuhifadhi mazingira kwa maslahi ya afya na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Kishapu Godwin Everygist amesema kuwa mamlaka imeanza mchakato wa ujenzi wa dampo la kisasa na la kudumu katika eneo la Sulagi.

Hata hivyo, kwa sasa wananchi wametakiwa kutumia vyema dampo la muda kwa kuhifadhi taka kwa ustaarabu.

"Katika kipindi hiki cha mpito, tunasisitiza uhifadhi sahihi wa taka kwenye dampo la muda, huku tukielekea kwenye Mji wa kisasa wenye miundombinu bora ya usimamizi wa taka," amesema Everygist.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa kila kaya kuhakikisha inakuwa na choo bora na salama ili kudhibiti uharibifu wa mazingira na magonjwa ya milipuko yanayochangiwa na uchafuzi wa mazingira.

Zoezi la usafi lililofanyika linahusisha maeneo muhimu ikiwemi Soko la Swalala, uwanja wa Shirecu, pamoja na dampo la muda, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kujenga utamaduni endelevu wa usafi katika Wilaya ya Kishapu.


Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Kishapu Godwin Everygist Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga akizungumza baada ya zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi Julai 26,2025

Soko la Swalala lililoko Mamlaka ya Mji Mdogo Mhunze Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga



































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com