Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SENYAMULE: VIJANA JENGENI MAISHA YENU KWA BIDII NA MAONO




Na Hellen M. Minja, Dodoma

Serikali mkoani hapa imetoa wito kwa vijana kuwa na maono ya maisha yao, kujitambua na kujikita katika kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza ndoto zao na kuchangia katika ujenzi wa taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, aliposhiriki hafla ya uzinduzi wa mafunzo ya ufundi stadi na ugawaji wa vifaa kwa vijana, iliyofanyika katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Chamwino, Julai 8, 2025.

Mhe. Senyamule amesema kuwa vijana wanaoshiriki mafunzo hayo ni miongoni mwa waliopata fursa adimu ambayo inapaswa kutumiwa kwa umakini na maarifa ili kubadili maisha yao na jamii kwa ujumla.

"Tunatamani kuona vijana wanaojitambua, wenye malengo na wanaofanya kazi kwa bidii kuyafikia,hii elimu mliyoipata haikuwepo zamani  watu walikuwa wakitembea kama vipofu lakini leo nyinyi mnaenda kama wenye maarifa. Itumieni vizuri fursa hii," amesema.

Mafunzo hayo yanatekelezwa chini ya mradi wa AHADI (Adolescent Health and Development Initiative), unaolenga kuongeza uelewa kuhusu afya ya uzazi kwa vijana wa miaka 10 hadi 24, sambamba na kuwawezesha kiuchumi.

Mradi huo unatekelezwa na mashirika ya World Vision Tanzania kwa kushirikiana na Tanzania Home Economics Association (TAHEA) katika majiji ya Dodoma na Dar es Salaam, kuanzia Aprili 2024 hadi Machi 2029.

Akizungumza kwa niaba ya TAHEA, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Bi. Lediana Mng’ong’o, alieleza kuwa zawadi zenye thamani ya shilingi milioni mbili kila moja zilitolewa kwa wahitimu wawili waliomaliza mafunzo ya ufundi stadi kwa mafanikio makubwa – mmoja kutoka fani ya upishi na mwingine kutoka urembo – ili kuwawezesha kuanzisha shughuli zao binafsi.

Naye Mhamasishaji wa vijana wa mradi huo, Bi. Scholastika Senga, alisema vijana waliotunukiwa zawadi walionesha moyo wa kujituma tangu mwanzo hadi mwisho wa mafunzo, hatua iliyowavutia wadhamini kuwapa vifaa hivyo kama motisha kwa wengine.

Mradi wa AHADI unaendelea kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa vijana nchini, kwa kuwawezesha kupata stadi muhimu za maisha, maarifa ya afya, na msingi wa kujitegemea kiuchumi.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com