
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Bw. Focus Mauki, akizungumza na waandishi wa habari wa Klabu ya Waandishi wa Habari Ruvuma (Ruvuma Press Club) wakati wa mafunzo ya ukaguzi yaliyofanyika mkoani Ruvuma.

Baadhi ya waandishi wa habari wa Klabu ya Waandishi wa Habari Ruvuma (Ruvuma Press Club) wakifuatilia mafunzo ya ukaguzi kwa klabu za waandishi wa habari, yaliyofanyika mkoani Ruvuma.
Na Regina Ndumbaro, Songea–Ruvuma
Waandishi wa habari kutoka Klabu za Waandishi wa Habari Mkoa wa Ruvuma wamepatiwa mafunzo ya ukaguzi yenye lengo la kuimarisha ushiriki wao katika kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma na kuhamasisha uwajibikaji wa mamlaka kwa wananchi.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Julai 23, 2025, katika ukumbi wa Songea Club, yakitekelezwa kwa usimamizi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) chini ya mpango mkakati wa kuimarisha uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau wa habari katika shughuli za ukaguzi wa serikali.
Watoa mada wakuu walikuwa ni wataalamu kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wakiwemo Bw. Nicolas Kilinga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NAOT – CEA Ruvuma, Bi. Sakina Mfinanga, Afisa Habari Mkuu, na Bw. Focus Mauki, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
Viongozi hao wameeleza kwa kina nafasi ya vyombo vya habari katika kuripoti ukaguzi wa serikali kwa uwazi, kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pamoja na kuandika taarifa zenye mchango katika kuchochea uwajibikaji na maendeleo ya jamii.
Miongoni mwa mambo yaliyofundishwa ni pamoja na mbinu za kisasa za ukaguzi wa ufanisi, uandaaji na uwasilishaji wa ripoti za ukaguzi, pamoja na namna bora ya kushirikiana kati ya waandishi wa habari na taasisi za umma.
“Lengo ni kuwajengea waandishi uelewa mpana juu ya wajibu wao kama daraja kati ya serikali na wananchi. Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuweka wazi taarifa za ukaguzi na kushinikiza utekelezaji wa mapendekezo ya CAG,” amesema Bw. Mauki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Ruvuma, Amon Mtega, ameishukuru serikali kupitia NAOT kwa kuandaa mafunzo hayo na kuahidi kuwa waandishi wa Ruvuma watazingatia mafunzo hayo kama sehemu ya kuimarisha taaluma na ushiriki wa jamii katika maendeleo.
“Tunashukuru kwa kutufikia huku Ruvuma. Tunakwenda kuyatumia maarifa haya kuhakikisha tunawajibika kwa taaluma na kusaidia jamii kujua kinachoendelea kuhusu matumizi ya fedha za umma,” alisema Mtega.
Social Plugin