Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Mkoa wa Katavi umeendelea kunufaika na maboresho ya huduma za afya chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 41 zimetolewa kwa kipindi cha miaka mitano kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na huduma za afya katika ngazi zote.
Akizungumza katika mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa miradi ya afya mkoani humo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amesema fedha hizo zimetumika kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Hospitali 4 za Wilaya, vituo vya afya 11, zahanati 47 na ukarabati wa Hospitali Kongwe ya Manispaa ya Mpanda pamoja na vituo vingine vya kutolea huduma.
Mrindoko ameeleza kuwa idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka 102 mwaka 2021 hadi 161 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 36.64, hali inayoashiria dhamira ya dhati ya Serikali kufikisha huduma bora karibu na wananchi.
Kwa upande wa zahanati, Mkuu huyo wa Mkoa amesema zimeongezeka kutoka 80 mwaka 2021 hadi 127 mwaka 2025, wakati vituo vya afya vimepanda kutoka 17 hadi 28 katika kipindi hicho, hatua inayosaidia kupunguza msongamano katika hospitali za wilaya.
Kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Mrindoko amebainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 18 zilitumika kukamilisha majengo ya kisasa kama vile huduma za wagonjwa wa nje, jengo la dharura (EMD), ICU, dialysis na nyumba za watumishi, pamoja na ununuzi wa mashine za CT-Scan, digital X-Ray na vifaa tiba vya kisasa.
Ameongeza kuwa hospitali hiyo sasa inatoa huduma za kibingwa ikiwemo upasuaji wa hali ya juu, mifupa, afya ya uzazi, magonjwa ya ndani, huduma za dharura pamoja na masuala ya pua, koo na sikio, hivyo kupunguza sana rufaa za wagonjwa kwenda nje ya mkoa.
Aidha, bajeti ya dawa mkoani humo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 2.98 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 3.38 mwaka 2024, ongezeko la asilimia 11.8, huku upatikanaji wa dawa ukifikia wastani wa asilimia 94 kufikia Juni 2025.
Huduma za dharura kwa wajawazito zimeimarika pia, ambapo ameeleza kuwa vituo vinavyotoa huduma hizo (CEmONC) vimeongezeka kutoka 8 hadi 14 kati ya 2021 na 2025. Aidha, idadi ya akina mama wanaojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kutoka 40,269 hadi 48,322 katika kipindi hicho.
Vilevile, idadi ya magari ya wagonjwa (ambulance) imeongezeka kutoka 10 hadi 17, hatua ambayo Mkuu wa Mkoa alisema imeongeza ufanisi wa uhamishaji wa wagonjwa kutoka ngazi ya zahanati hadi hospitali za wilaya na hospitali ya rufaa ya mkoa.
Social Plugin