
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana
na Wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe.
Patrobas Katambi, ametimiza ahadi yake kwa kuikabidhi timu ya Stand United
kiasi cha shilingi milioni tano (5,000,000/=), alizokuwa ameahidi iwapo timu
hiyo ingeshinda mchezo wake wa awali dhidi ya Fountain Gate FC.
Licha ya Stand United kupoteza
mchezo huo uliochezwa juzi, katika uwanja wa CCM Kambarage Mhe. Katambi
ameonesha mfano wa kuigwa kwa kutimiza ahadi yake, ambapo amekabidhi fedha hizo
kwa mlezi wa timu hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius
Mtatiro.
Akizungumza wakati wa kukabidhi
fedha hizo, leo Julai 7, 2025 Mhe. Katambi amesema alitoa ahadi hiyo kama
sehemu ya kuwahamasisha vijana kupambana na kuonesha ushindani, lakini pia
kutambua juhudi na nia njema ya timu hiyo katika kuinua tasnia ya michezo
mkoani Shinyanga.
Katika hatua nyingine, Mhe. Katambi
ametangaza ahadi mpya ya kutoa shilingi Milioni Kumi (10,000,000/=) endapo
Stand United itaibuka na ushindi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Fountain
Gate FC na kufanikisha kupanda Ligi Kuu ya NBC msimu ujao, huku akiwataka
mashabiki wa soka mkoani humo kuendelea kuipa sapoti timu yao.
“Ninawaamini vijana wetu, naamini
morali iko juu na watapambana kwenye mchezo wa marudiano, nipo hapa kama mbunge
wa jimbo la Shinyanga Mjini kuwahamasisha na kuhakikisha ndoto ya kurejea Ligi
Kuu inatimia,” amesema Mhe. Katambi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga na mlezi wa Stand United, Wakili Julius Mtatiro, amemshukuru Mhe. Patrobas
Katambi kwa kuendelea kuwa bega kwa bega na timu hiyo, akisema mchango wake ni
chachu ya maendeleo ya michezo mkoani humo, huku akiahidi kufanya vizuri katika
mchezo unaofuata na kuhakikisha furaha ya wana Shinyanga inarejea kwa kurudi
kushiriki kwenye ligi kuu Tanzania Bara.
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
Social Plugin