Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

INEC YATUPA KARATA YA UWAJIBIKAJI KWA VYAMA VYA SIASA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025


Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefanya Mkutano wa Kitaifa na Vyama vya Siasa leo Julai 27, 2025 jijini Dodoma, ambapo imetangaza kuongezwa kwa majimbo mapya nane ya uchaguzi kwa upande wa Tanzania Bara, na hivyo kufanya jumla ya majimbo kufikia 272 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufani) Jacobs Mwambege, amesema mabadiliko hayo ni sehemu ya maboresho ya mfumo wa uchaguzi ili kuendana na ongezeko la watu na mahitaji ya usawa wa uwakilishi wa wananchi.

Jaji Mwambege ameongeza kuwa Tume pia imeongeza kata tano mpya, na sasa Tanzania Bara ina jumla ya kata 3,960, ikiwa ni juhudi za kurahisisha usimamizi wa uchaguzi katika ngazi za msingi na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kushiriki kwa ufanisi.

“Mabadiliko haya yamezingatia takwimu rasmi za idadi ya watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), maeneo ya kijiografia pamoja na maoni ya wadau wa uchaguzi waliowasilishwa kwa Tume katika vikao mbalimbali vya mashauriano,” amefafanua Jaji Mwambege.

Akitaja hatua zilizokamilishwa, Jaji Mwambege alisema Kalenda ya Uchaguzi tayari imezinduliwa rasmi Julai 26, 2025. Kulingana na ratiba hiyo, utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea utafanyika kuanzia Agosti 9 hadi 27, huku kampeni zikianza Agosti 28 na kufikia tamati Oktoba 27.

Amesisitiza kuwa kila hatua ya maandalizi imekuwa ikitekelezwa kwa uwazi, ushirikiano na ushauriano na wadau wakuu wa uchaguzi, hususan vyama vya siasa, ili kujenga mazingira ya uchaguzi wa haki, huru, na unaoaminika.

Katika mchango wao, viongozi wa vyama vya siasa waliopata nafasi ya kutoa maoni wakati wa mkutano huo wameipongeza INEC kwa kuendesha mchakato wa maandalizi ya uchaguzi kwa uwazi na kwa kuwashirikisha vyama tangu hatua za awali.

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF, amesema maandalizi ya mwaka huu yamekuwa bora zaidi ikilinganishwa na chaguzi zilizopita, hasa kwa kuwa Tume imetoa daftari la kudumu la wapiga kura kwa wakati na kuanzisha utaratibu wa kutoa taarifa kwa uwazi.

“Tumefanya mapitio ya Ilani ya Uchaguzi na sasa tunaendelea na mafunzo ya maadili na mikakati ya kampeni kwa wagombea wetu kote nchini. Tumewaandalia vikosi kazi vya kimkakati kutoka ngazi ya taifa hadi mikoa ili kuhakikisha tunashiriki kwa ufanisi,” amesema Prof. Lipumba.

Aidha, amesisitiza kuwa uchaguzi siyo uwanja wa matusi bali ni jukwaa la hoja, na CUF imeunda kamati maalum ya maadili kuhakikisha wagombea wake wanazingatia nidhamu wakati wote wa kampeni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ADA-TADEA, Juma Ally Khatib, ameeleza kuwa chama chake kimeweka mikakati mahsusi ya kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika uchaguzi kwa kutoa mafunzo ya uongozi, kuondoa vikwazo vya kisiasa na kijamii, pamoja na kuwasaidia kwa rasilimali.

“Tunaamini ushiriki wa wanawake na vijana si mapambo, bali ni msingi wa mabadiliko na demokrasia jumuishi. Tutahakikisha wanapata nafasi ya kugombea majimbo ya wazi na kushiriki kikamilifu katika mchakato huu,” amesema.

Mkutano huo wa kitaifa umeonesha dhamira ya pamoja kati ya Tume ya Uchaguzi na wadau wa kisiasa katika kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2025 unafanyika kwa misingi ya utulivu, ushirikiano na heshima ya demokrasia.










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com