Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na Mwenyekiti wa Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM), Dkt. Jim Yonazi, ameongoza kikao muhimu cha TNCM kwa ajili ya kupitisha maboresho ya bajeti ya utekelezaji wa programu zinazofadhiliwa na Mfuko wa Dunia (Global Fund) kwa mzunguko wa saba (GC7) wa miaka 2024 hadi 2026.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 10 Julai 2025 katika Jengo la Tume ya Ushindani, jijini Dar es Salaam, kikilenga kupitia na kuidhinisha marekebisho ya bajeti ya programu dhidi ya magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI — maeneo matatu yenye umuhimu wa kipekee kwa afya ya jamii ya Watanzania.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, wakiwemo wawakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Wizara ya Afya, pamoja na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).
Vilevile, walikuwapo wawakilishi kutoka Bohari ya Dawa (MSD), wakaguzi wa ndani wa Mfuko (Local Fund Agent - LFA), Sekretarieti ya TNCM, pamoja na Asasi za Kiraia (Non-State Actors – NSAs).
Mashirika ya kimataifa kama Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS), pamoja na Wadau wa Maendeleo kutoka Serikali ya Marekani na Ubalozi wa Uingereza, walishiriki kutoa mchango wao katika mchakato huo wa kupanga bajeti kwa ufanisi na ushirikishwaji wa pande zote.
Kupitia kikao hicho, TNCM inaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa yanayotishia maisha ya wananchi, kwa kuhakikisha rasilimali za kimataifa zinatumika kwa uwazi, tija na ufanisi mkubwa.

Social Plugin