Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BALOZI POLEPOLE AJIUZULU NAFASI YAKE CUBA, AWASILISHA BARUA KWA RAIS SAMIA




Na Dotto Kwilasa

Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ametangaza kujiuzulu rasmi nafasi yake ya kidiplomasia kupitia taarifa aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram na mitandao mingine ya kijamii na hivyo kusitisha jukumu lake la kuiwakilisha Tanzania katika taifa hilo la Amerika ya Kusini.

Katika taarifa hiyo, Balozi Polepole amesema kuwa amechukua hatua hiyo kwa hiari na kwa kufuata utaratibu rasmi, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha barua kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 “Nimemwandikia barua Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuomba kuachia rasmi nafasi ya uwakilishi wangu kama Balozi,” ameandika Polepole katika chapisho lake.




Akiwa balozi, Polepole alihusika katika kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Cuba, hususan katika sekta za afya, elimu na diplomasia ya maendeleo. 

Kabla ya uteuzi huo wa kidiplomasia, Polepole aliwahi kushika nafasi mbalimbali serikalini na CCM ikiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa kuteuliwa.

Licha ya kubainisha sababu kamili za kujiuzulu kwake kuwa ni kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi wa Tanzania, taarifa hiyo imeibua hisia mbalimbali mitandaoni, huku baadhi ya wananchi wakimpongeza kwa uwazi na uamuzi wake wa hiari.

Hatua hii ya kujiuzulu inakuja wakati serikali ikiendelea na maboresho katika mfumo wa uwakilishi wa kidiplomasia, ambapo mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania maeneo mengi duniani wanasisitizwa  kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwazi na uzalendo.

Mpaka sasa, haijafahamika rasmi ni nani atachukua nafasi hiyo ya uwakilishi wa Tanzania nchini Cuba, lakini matarajio ya Watanzania ni kuona mwendelezo wa ushirikiano imara kati ya mataifa haya mawili.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com