
📌Ni katika Ziara yake kwenye vituo vya kuzalisha umeme kwa gesi asilia vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II
📍Asema ni jitihada za uwekezaji uliofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
📌Aipongeza TANESCO kwa kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika.
Na Mwandishi wetu - Dar es salaam
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Tanzania kwa sasa ina umeme wa kutosha, hali inayoashiria mafanikio ya juhudi za uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo wakati wa ziara yake katika vituo vya kuzalisha umeme kwa gesi asilia vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II, Dkt. Biteko amesema kuwa kukamilika kwa miradi mikubwa ya kuzalisha umeme, ikiwemo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha megawati 2,115, kumeiwezesha nchi kuwa na akiba ya umeme wa kutosha.
“Nataka niseme mbele yenu ndugu zangu, Mheshimiwa Rais Samia ndiye kinara wa haya yote. Amefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati. Bajeti ya Wizara yetu imeongezeka hadi Shilingi trilioni 2.3. Lengo lake kuu ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa licha ya kuwepo changamoto katika baadhi ya maeneo, hali ya upatikanaji wa umeme imeendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi za TANESCO.
Katika kuhakikisha mahitaji ya nishati yanakwenda sambamba na ongezeko la watu na matumizi, Dkt. Biteko amesema TANESCO ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa umeme katika Kituo cha Kinyerezi III, kutoka megawati 600 hadi megawati 1000.
Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza TANESCO kwa maboresho yanayoendelea kufanywa katika huduma kwa wateja, hususan usimamizi wa dharura za umeme na uboreshaji wa kituo cha huduma kwa simu, ambacho sasa kinahudumia wananchi bila malipo.
“Nawapongeza kwa kuonyesha uharaka katika kushughulikia changamoto za umeme. Pia ni hatua nzuri mlivyoboreshwa kituo cha miito ya simu ili wananchi wapate huduma bila gharama,” ameongeza.




Social Plugin