FISI AVAMIA KIJIJI AKILIA KAMA BINADAMU, AJERUHI KATIBU WA CCM NA WANAZENGO, NYAMA YAGOMBANIWA

NB- Picha ya Fisi haihusiani na fisi aliyejeruhi wananchi

Na Lucas Raphael  – Tabora

Kwa zaidi ya dakika 45, wakazi wa Kijiji cha Bulumbela, Wilaya ya Igunga, walikumbwa na taharuki isiyoelezeka huku wakishuhudia fisi mmoja akirukia kila mtu aliyemkaribia, akitoa sauti zisizo za kawaida zilizofanana kabisa na kilio cha binadamu.

Sauti hizo zilitawala anga ya kijiji hicho Julai 14, 2025, majira ya saa mbili asubuhi, kabla ya fisi huyo kumshambulia mtu wa kwanza na kuanza kujeruhi kadhaa kwa mpigo.

Katika tukio hilo la kushtua, watu wanne walijeruhiwa vibaya na fisi huyo, akiwemo Maganga Nkwande ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbuyuni, na Busongo Malekela, Katibu wa CCM Tawi la Bulumbela. Wengine walioumia ni wakazi wa kijiji hicho, Juma Masanilo na Tatu Kabeya.

Kwa mujibu wa Idd Makalo, Mtendaji wa Kijiji cha Bulumbela, fisi huyo aliibuka ghafla katika makazi ya watu na kuanza kushambulia kwa ukali na kasi isiyotarajiwa.

“Alikuwa anarukia kila mtu, hakuchagua. Alikuwa na nguvu na alilia kama binadamu... ni hali ambayo haijawahi kutokea hapa kwetu,” amesema Mtendaji huyo.

Wananchi waliokusanyika baada ya kusikia mayowe ya majeruhi, walimkabili fisi huyo kwa kutumia silaha za jadimapanga, mikuki, na mashoka na hatimaye wakafanikiwa kumuua.

Kilichoshangaza zaidi, baada ya kuangushwa, baadhi ya wananchi waliamua kugawana viungo vya fisi huyo na kuondoka navyo, wakisema hakuwa fisi wa kawaida.

Mrisho Juma na Fadhili Isaya, mashuhuda wa tukio hilo, wamesema mapambano hayo yalikuwa magumu na ya kutisha.
“Alikuwa anakimbia na kurudi ghafla… alikuwa akilia kama binadamu, hadi tukashindwa kuelewa huyu ni fisi wa aina gani,” amesema Mrisho.

Wananchi hao wamesema Fisi huyo walipambana naye kwa zaidi ya dakika 45 ambapo alikuwa akirukia kila mtu aliyemsogelea, hata hivyo mwananchi mmoja alifanikiwa kumkata na shoka kichwani hadi kuanguka na kufa pale pale.

“Kwa kweli huyu Fisi siyo wa kawaida kwani wakati tukipambana naye alikuwa akipiga kelele kama binadamu na ndiyo maana tumeamua kugawana viungo vyake vyote”.

Emanuel Mnanka, Kaimu Mkuu wa Idara ya Maliasili na Hifadhi ya Mazingira Wilaya ya Igunga, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa walipokea taarifa kutoka kwa Mtendaji wa kijiji wakati wakijiandaa kwenda eneo la tukio.

Majeruhi wote walipelekwa Kituo cha Afya cha Ziba na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Igunga kwa ajili ya kupata chanjo dhidi ya wanyama wakali, hasa ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Dkt. Lucia Kafumu, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Igunga, amesema hali za majeruhi zinaendelea vizuri na walipatiwa huduma zote muhimu za kitabibu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com