
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Bw.Chrispin Francis Chalamila akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la ofisi hizo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Juni 25, 2025
Na Sumai Salum-Kishapu
Wananchi Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wamepongeza jitihada za serikali ya awamu ya sita za ujenzi miundombinu ya jengo la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani humo.
Pongezi hizo zimetolewa Juni 26,2025 baada ya uzinduzi wa jengo lenye thamani ya Tsh.Milion 438 lilolofanywa Juni 25,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bw.Crispin Francis Chalamila.
Bw.Amos Masunga mkaazi wa mtaa wa Mwasele 'B' amesema uwepo wa jengo la Taasisi hiyo usiwe sababu ya utoaji elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya upingaji rushwa na mahali wanapopaswa kupeleka malalamiko yao pindi wanapokosa huduma zilizo haki zao kisheria wakihitajika kutoa Rushwa.
"Jengo hili linafaida zaidi kwetu wananchi endapo TAKUKURU watafanya kazi zao kwa mwongozo waliowekewa hivyo watoke ofsini na kuwandea wananchi ili kuwaelimisha kuhusu maana ya Rushwa na viashiria vya rushwa hasa kundi la wanawake na wasichana wanaokutana na changamoto zaidi ya kuombwa rushwa ya ngono ili wapate kazi na wengine kupandishwa cheo"ameongeza Masunga
Ludovic John mkazi wa Mhunze na John Amos mkazi wa Ikonda wamesema kuwa uwepo wa ofisi hiyo unafaida kubwa kuliko hapo awali kulingana na eneo jengo lilipokuwa kwani inawapa wananchi moyo wa kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za Rushwa wakiwa na uhakika wa usiri.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo hilo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Chrispin Francis Chalamila amesema uwepo wa jengo hilo ni hatua kubwa ya kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa ngazi ya jamii.
“Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za TAKUKURU kote nchini hivyo tunatambua umuhimu wa taasisi hii, na ni jukumu la kila mwananchi kulitumika jengo hili kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria au vitendo vya rushwa iliyo adui mkubwa wa maendeleo ya taifa letu,” amesema Chalamila.
Amesisitiza umuhimu wa kuchagua wagombea waadilifu kwa kuwa hao ndio watakaoshirikiana na wananchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo katika kuleta maendeleo ikiwa kura ni tiketi ya maendeleo na uwajibikaji.
“Tukikubali kupokea rushwa kutoka kwa wagombea, ni sawa na kukataa maendeleo yetu wenyewe. Mara nyingi waliotoa rushwa hushindwa kuwajibika ipasavyo na badala yake hutanguliza maslahi yao binafsi,” ameongeza.
Amehimiza maafisa wa TAKUKURU kuongeza mbinu za ushirikishaji jamii kwa njia ya elimu, vikundi vya sanaa, na klabu mashuleni ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya rushwa.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, na Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo, ameipongeza serikali kwa mpango wake wa dhati wa kuimarisha taasisi hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
“TAKUKURU ni chombo cha haki kwa wananchi. Tunaposhuhudia nidhamu ikirejeshwa miongoni mwa watumishi na wafanyabiashara, tunapata matumaini ya taifa lenye uwajibikaji na maendeleo na hii itaongeza ufanisiwa utendaji kazi kwa watumishi wa Taasisi hii kwa kuboreshewa mazingira ya kazi zao,” amesema Butondo.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, amesema jengo hilo ni kichocheo cha haki na uwazi katika jamii, huku akiwataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kupinga rushwa kwa kutoa taarifa kwa wakati.
“Tunawashukuru sana TAKUKURU kutuheshimisha kwa kutujengea jengo hili hapa Kishapu ni hatua ya kupongezwa hivyo Wananchi mnapaswa kutumia fursa hii kwa kutoa taarifa na sasa tumeboreshewa usiri tofauti na hapo awali kutokana na mazingira ya ofisi ombi langu muendelee kuelimishwa kuhusu rushwa hasa tunapoelekea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani,” amesema Masindi.
Mkurugenzi wa Hati Milki wa TAKUKURU, Eng. Dkt. Emmanuel Kiyabo, ameeleza kuwa serikali imeendelea kuongeza bajeti ya taasisi hiyo kila mwaka kwa lengo la kuboresha miundombinu na mazingira ya kazi.
“Ujenzi wa jengo hili ulianza Januari 27, 2024 na kukamilika Julai 16, 2025 kwa asilimia 100. Ujenzi ulijumuisha jengo kuu, ukuta na miundombinu mingine ya ofisi,” ameeleza.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeongeza bajeti ya TAKUKURU kwa mafanikio makubwa. Kuanzia bilioni 1.5 mwaka wa fedha 2021/22, bajeti imeongezeka hadi bilioni 6.0 mwaka 2025/26 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa majengo mapya,ukarabati wa majengo ya zamani pamoja na ujenzi wa uzio kwenye ofisi zisizo na uzio.
Ofisi ya TAKUKURU Kishapu iko katika Mtaa wa Mwasele ‘B’, ndani ya Mamlaka ya Mji Mdogo Kishapu, tofauti na awali ambapo ilikuwa Mtaa wa Makambini katika majengo ya zamani ya Shirecu huku Kauli mbiu ya TAKUKURU ikibaki kuwa: "Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu Tutimize Wajibu Wetu."






















Social Plugin