Katibu wa wilaya CCM Masasi Ndugu Hemed Said Ferej akimkabidhi fomu mwanachama kwa lengo la kugombea nafasi za ubunge na udiwani wilayani humo
Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Masasi wamejitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea ubunge na udiwani (viti maalum) kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Fomu kwa wagombea wa nafasi ya ubunge kwa majimbo ya Masasi, Ndanda na Lulindi zimetolewa na Katibu wa CCM Wilaya ya Masasi, Ndugu Hemed Said Ferej, katika ofisi kuu ya chama wilayani humo.
Kwa upande wa wagombea wa viti maalum vya udiwani, fomu hizo zinatolewa na Katibu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Masasi, Bi Hilda Silvester Mizengo.
Baadhi ya wanachama waliokwisha jitokeza kuchukua fomu ni pamoja na Hadija Utukuru (Jimbo la Lulindi), Martin Mkanga (Lulindi), Bwana Hausi (Lulindi), Abduli Chionda (Masasi Mji) na Dkt. Leonard Akwilapo (Masasi Mji).
Hali hiyo inaashiria mwamko mkubwa wa kisiasa ndani ya chama hicho wilayani Masasi.
Akizungumza na waandishi wa habari Katibu wa CCM Wilaya ya Masasi Ndugu Hemed Said Ferej, ametoa wito kwa wanachama wote wenye sifa na nia ya kugombea nafasi hizo kujitokeza mapema na kuchukua fomu kabla ya muda wa mwisho kufika.
Ametoa rai hiyo akiwaasa wanachama kuzingatia utaratibu, nidhamu, na misingi ya chama katika mchakato mzima wa kuchukua na kurejesha fomu.

Social Plugin