Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KARIBU KILI - FAIR 2025 YALETA TUMAINI JIPYA KWA SEKTA YA UTALII


Na Woinde Shizza , Arusha 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema sekta ya utalii ni nguzo muhimu ya uchumi wa taifa na kuitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuimarisha mikakati ya kisasa ya kuitangaza Tanzania kimataifa.

Dkt. Biteko aliyasema hayo jana jijini Arusha wakati akifungua rasmi maonesho ya kimataifa ya Karibu Kili-Fair, yanayofanyika katika viwanja vya Magereza - Kisongo.

Alisema kuwa sekta ya utalii inachangia asilimia 7.9 ya pato la taifa, na ni miongoni mwa sekta zenye mchango mkubwa katika ajira na kukuza uchumi wa nchi.

"Serikali inaendelea kutekeleza programu mbalimbali, ikiwemo Royal Tour, ambazo zimeleta matokeo chanya katika kuitangaza Tanzania kimataifa na kuvutia watalii na wawekezaji," alisema Dkt. Biteko.

Aidha, aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na waandaaji na washiriki wa maonesho hayo kwa juhudi zao katika kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko alizitaka taasisi husika kuandaa mikakati madhubuti ya kuendeleza mazao ya utalii yenye tija na kutumia teknolojia ya TEHAMA katika kutangaza vivutio vya nchi, akisisitiza ubunifu kama nyenzo ya kuongeza ushindani katika soko la kimataifa.

Aliwahimiza pia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta hiyo, akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuondoa vikwazo na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, aliiomba Serikali kulitambua eneo la Magereza - Kisongo kuwa maalum kwa maonesho ya kimataifa ya utalii, ili kuvutia wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Makonda pia alipendekeza muda wa maonesho hayo uongezwe kutoka siku tatu hadi siku tano au saba, ili kutoa fursa pana kwa washiriki kuonyesha bidhaa na huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta ya utalii

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com