Na Regina Ndumbaro Tunduru-Ruvuma
Katika mnada wa kwanza wa zao la ufuta uliofanyika kijiji cha Mchesi, Tarafa ya Lukumbule, Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, jumla ya tani 1,273.487 za ufuta zenye thamani ya Shilingi bilioni 3.1 ziliuzwa kupitia Chama cha Msingi cha Ushirika cha Mruji Amcos.
Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru, Marcelino Mrope, ameeleza kuwa bei ya chini ilikuwa Sh.2,410 kwa kilo, ya juu Sh.2,460, na bei ya wastani ilikuwa Sh.2,439, ikiwa ni pungufu ikilinganishwa na msimu uliopita.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Simon Chacha, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuweka mazingira bora ya soko ambayo yamewanufaisha wakulima.
Amesisitiza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani utaendelea kusimamiwa ili kuimarisha mauzo ya mazao.
Aidha, amewasihi wakulima kutumia taasisi za kifedha kupokea malipo yao na kutumia fedha wanazopata kuboresha maisha badala ya kuzitumia kwa anasa.
Kaimu Afisa Kilimo wa Wilaya ya Tunduru, Gallus Makwisa, amewapongeza wakulima kwa kuvuka lengo la uzalishaji kutoka tani 4,000 mwaka 2023 hadi tani 8,000 mwaka 2024.
Amesema halmashauri kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Ruvuma imesambaza tani 8,000 za mbegu kwa wakulima katika kata 36 ili kuongeza uzalishaji wa ufuta wenye ubora na ushindani wa soko.
Kwa upande wake, Afisa Masoko wa TAMCU, Stella Msengi, amesema msimu wa 2024/2025 umeongeza uzalishaji hadi kilo 8,774,621, sawa na ongezeko la asilimia 60.09.
Amebainisha kuwa lengo la msimu wa 2025/2026 ni kukusanya kilo 12,811,100 na kuwaomba wakulima waendelee kupeleka mazao yao kwenye vyama vya msingi ili kunufaika na mfumo wa mnada.
Social Plugin