Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TRA SHINYANGA YATOA ELIMU YA KODI KWA WANAFUNZI WA CHUO CHA VETA


Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga imeendesha semina ya elimu ya ulipaji kodi kwa wanachuo wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea uelewa vijana kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi.

Semina hiyo imefanyika leo Juni 25, 2025 katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga kilichopo manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza wakati wa semina hiyo, Afisa wa kodi kutoka TRA Shinyanga Semeni Mbeshi, amesema lengo ni kuwajengea msingi mzuri wa kizalendo vijana wanaotarajia kuingia kwenye soko la ajira na kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao.

Ameongeza kuwa elimu hiyo ni endelevu na inalenga kujenga taifa la watu waaminifu katika ulipaji wa kodi, huku akisisitiza matumizi ya Mashine za  risiti za Kielektroniki (EFD)  kwa wafanyabiashara na kutoa na kudai risiti pindi wanaponunua bidhaa.

“Haki ya mlipa kodi ni kuaminiwa pindi anapofika kwenye ofisi za TRA kwa ajili ya kufanyiwa makadirio yanayoendana na biashara yake, ni wajibu wa kila mfanyabiashara kutoa taarifa ya ufanyaji wa biashara kwa mamlaka ya mapato TRA, Mashine za  risiti za Kielektroniki (EFD)  zinasaidia kuweka rekodi sahihi ya kumbukumbu ya biashara kwa muda wa miaka 5, lakini kodi hiyo inakwenda moja kwa moja kwenye mfuko wa serikali na kuwezesha maendeleo kwenye taifa letu”, amesema Semeni Mbeshi.

Kwa upande wake, Mkufunzi katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga, Emili Shirima amesema vitendo vya baadhi ya watu kutumia vishoka kujipatia huduma za kikodi si sahihi na ni hatari kwa uchumi wa taifa, na amewataka wanachuo kujiepusha na tabia hizo mara watakapoingia kwenye shughuli za uzalishaji mali.

Baadhi ya wanachuo walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru TRA kwa kuwapa elimu hiyo muhimu, wakisema itawasaidia  mara baada ya kuhitimu na kuanzisha biashara au shughuli za kujitegemea na kuongeza kuwa sasa wanaelewa kwamba ulipaji wa kodi unasaidia huduma za jamii kama afya, elimu na miundombinu.

Afisa wa kodi kutoka TRA Shinyanga Semeni Mbeshi akizungumza wakati wa mafunzo hayo.







Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo.


















Mkufunzi katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga, Emili Shirima akizungumza mara baada ya elimu hiyo kutolewa. 




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com