
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia ofisi yake ya Wilaya ya Shinyanga, imetoa mafunzo maalum kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji juu ya namna bora ya kukabiliana na matukio ya uvamizi wa nyuki kwa lengo la kulinda maisha ya wananchi na wahanga wa mashambulizi hayo.
Mafunzo
hayo yametolewa kufuatia kuongezeka kwa visa vya nyuki kuvamia makazi ya watu
na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo majeraha na hata vifo, hali ambayo
imeleta hofu kwa baadhi ya wakazi wa maeneo ya vijijini na mijini.
Akizungumza
wakati wa kutoa elimu hiyo, Mtaalam wa masuala ya nyuki Barnabas Salun,
ameeleza hatua sahihi za kufuata wanapokabiliana na matukio ya watu
kushambuliwa na nyuki. na kusisitiza umuhimu wa kutumia vifaa vya kisasa vya
kujikinga pamoja na kuchukua tahadhari ili kuokoa maisha bila kuweka maisha yao
pia hatarini.
"Katika uokoaji wa
tukio la nyuki, usalama wa mtaalamu wa uokoaji ni jambo la kwanza kuzingatia.
Tumejifunza mbinu sahihi za kutumia vifaa, namna ya kutambua aina ya nyuki, na
hatua za haraka za msaada kwa wahanga," amesema Salun.
Kwa upande wake, Afisa Uelimishaji kutoka TFS, Fanael Sumali, ametoa wito
kwa wananchi kuacha tabia ya kufuga nyuki kiholela katika makazi ya watu,
akisema kuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha ya watu wasiokuwa na uelewa wa
masuala ya nyuki.
"Tunahimiza watu
wafuge nyuki katika maeneo yaliyotengwa na kufuata taratibu za kitaalamu.
Ufugaji holela unachochea migogoro kati ya binadamu na nyuki," alisema Sumali.
Wakizungumza mara baada ya kupatiwa elimu hiyo maafisa na
askali wa jeshi la zimamoto na uokoaji Wilayani Shinyanga wakaeleza changamoto wanazokumbana
nazo katika uokoaji wa matukio ya nyuki kushambulia watu huku wakiahidi kutumia
elimu hiyo waliyoipata kuboresha huduma zao za uokoaji.
Afisa Mhifadhi
Mwandamizi kutoka TFS Wilaya ya Shinyanga, Mhifadhi Fabiani Balele, amesema
lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa na uwezo wa vikosi vya uokoaji katika
kukabiliana na matukio ya nyuki, kutokana na ongezeko la matukio hayo katika
maeneo mbalimbali.
"Tumeona
umuhimu wa kushirikiana na taasisi nyingine kama zimamoto ili kwa pamoja tuweze
kuhakikisha usalama wa jamii yetu dhidi ya majanga yanayosababishwa na nyuki,
hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi na mwingiliano wa binadamu na maeneo
ya asili ya nyuki," amesema Mhifadhi Fabiani Balele.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha jamii
inaishi kwa usalama sambamba na uhifadhi endelevu wa misitu na viumbe hai
waliopo ndani yake.

Social Plugin