Na Dotto Kwilasa, DODOMA
Serikali imetangaza msimamo wake dhidi ya waajiri wanaowatumia watoto kama nguvu kazi, ikisisitiza kuwa hakuna nafasi ya kuendeleza vitendo vya kuwadhalilisha watoto kwa kuwanyima haki ya kufurahia utoto wao, heshima na utu wao.
Kauli hiyo imetolewa June 12,2025 na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji Watoto, ambapo alisisitiza kuwa taifa lina wajibu wa kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye staha.
“Watoto ni hazina ya taifa, na wanahitaji malezi bora. Serikali haitakubali kuona mtoto akifanya kazi hatarishi au kuingizwa kwenye ajira isiyo rasmi,” amesema Waziri Katambi na kubainisha kuwa Serikali imeongeza magari ya ukaguzi kwa ajili ya kudhibiti na kufuatilia ajira haramu za watoto.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, mtoto mwenye umri chini ya miaka 14 haruhusiwi kabisa kufanya kazi ya kuajiriwa.
Hata hivyo, watoto wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17 wanaruhusiwa tu kufanya kazi nyepesi zisizoathiri afya yao, mahudhurio shuleni, au maendeleo yao ya kielimu na kimwili.
Waziri Katambi ameonya dhidi ya ajira zenye hatari kama kilimo kinachotumia kemikali, uchimbaji wa madini, kazi za usiku au zinazohitaji nguvu kubwa, akizitaja kuwa ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Groly Emmanuel, alieleza kuwa watoto milioni 160 duniani wanatumikishwa, huku zaidi ya asilimia 70 wakijihusisha na kazi katika sekta ya kilimo – hasa vijijini ambako ukaguzi wa ajira ni mdogo.
“Katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, tumeshuhudia kupungua kwa kiwango cha utumikishwaji wa watoto kwa asilimia 10 tangu mwaka 2020, lakini bado changamoto ni kubwa,” amesema Emmanuel.
Ameongeza kuwa asilimia 24.9 ya watoto hao wanashiriki katika kazi mbaya zaidi kama migodini, usafirishaji haramu, na ajira zenye unyanyasaji wa kingono au kimwili.
Akiweka msisitizo zaidi, Emmanuel amesema mtoto wa kike bado yuko hatarini zaidi, hasa katika kazi za ndani ambazo hufanywa kwa siri na kukosa ulinzi wa kisheria. Alitoa wito kwa wazazi kutambua kuwa jukumu la mtoto ni kusoma, si kutafuta kipato cha familia.
“ILO inapendekeza kuimarisha ajira zenye staha kwa wazazi, mifumo ya hifadhi ya jamii, elimu ya jamii kuhusu madhara ya ajira kwa watoto, pamoja na kutungwa na kutekelezwa kwa sheria kali dhidi ya wanaokiuka haki za watoto,” amesisitiza.
Naye Kamishna wa Kazi, Susan K. Mkangwa, alisema Serikali kupitia Idara ya Kazi imepanga kufanya kaguzi maalum katika mashamba, migodi na maeneo mengine ili kubaini ajira haramu kwa watoto na kuchukua hatua kali kwa waajiri wanaohusika.
“Tutazindua kampeni maalum za uhamasishaji ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya utumikishwaji watoto. Lengo letu ni kuhakikisha hakuna mtoto anayelazimishwa kufanya kazi yoyote kinyume cha sheria,” alisema Kamishna Mkangwa.
Ameongeza kuwa Tanzania imeridhia rasmi Mikataba Miwili Mikubwa ya ILO—Mkataba Na. 138 unaoweka umri wa chini wa kuajiriwa, na Mkataba Na. 182 unaopinga aina mbaya zaidi za ajira kwa watoto.
Kupitia mikataba hiyo, Serikali imesisitiza kuwa watoto ni raia wa kesho wanaopaswa kulindwa, kufundishwa, na kulelewa kwa upendo na uangalizi wa karibu.
Social Plugin