
Na Hamida Kamchalla, TANGA.
PAMOJA na jitihada za serikali kupambana na janga la uvuvi haramu nchini, bado inakabiliwa na janga hilo sambamba na utoroshwaji wa mazao ya uvuvi jambo ambalo linasababisha kama Wizara ya Uvuvi kuonekana haichangii ipasavyo katika pato la Taifa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi, Kitengo cha Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi, Dkt Baraka Sekadende wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau kilichoandaliwa na Shirika la Wildlife Conservation Society (WCS) la mkoani Tanga.
Aidha kikao hicho kimelenga kuazimisha shuhuli tofauti tofauti za kijamii zinazofanywa na mashirika na wadau ili kuboresha usimamizi na rasilimali za bahari.
Ameeleza kwamba katika ukanda wa pwani uvuvi umeendelea kukabiliwa pia na changamoto ya uduni wa miundombinu ya Uvuvi hususani mialo, chanja za kukaushia dagaa na uchakavu wa masoko ya samaki, "hii inapelekea upotevu wa mazao ya uvuvi na kupunguza kipato cha wavuvi".
Dkt. Sekadende amesema katika kuchangia pato la Taifa la Taifa pamoja na usalama wa chakula, "bado tupo chini sana katika ulaji wa samaki, Kidunia mtu mmoja anatakiwa kula kg 20 kwa mwaka, lakini sisi Tanzania tupo wastani wa kg 8 tu kwa mtu mmoja".
Amesema Wizara ina jukumu la kusimamia, kuhifadhi, kulinda na kuendeleza rasilimali za uvuvi, na katika kutekeleza jukumu hilo imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika binafsi kama WCS pamoja na jamii.
Kwa muktadha huo amewaomba wadau hao kuhakikisha Wizara inapata taarifa sahihi kuhusiana na mipango ya miradi inayotekelezwa kabla ya kuanza kwani itasaidia kupunguza migongano katika utekelezaji wa shuhuli zao.
"Hii pia itasaidia kupunguza matumizi ya nguvu kubwa ya fedha za wadau katika eneo moja, lakini vilevile itatoka nadfasi ya kujua aina ya shuhuli kwa kila mmoja wenu pindi tu alitolea mwengine kutaka kuanzisha aina hiyo mahali hapo" amesema.
Mratibu wa Shirika la Wildlife Conservation Society (WCS) Dkt. Johnson Mshana amesema wanafanya kazi katika Mikoa 13 nchini, lakini katika Programu ya kazi za baharini inafanya katika Mikoa ya Tanga, Dar es salaam, Mtwara na Unguja kwa upande wa Visiwani.
Amesema moja ya kazi ambayo wanaofanya katika Mkoa wa Tanga hasa Wilaya ya Mkinga ni kusaidia jamii za wavuvi kutengeneza mipango ya usimamizi wa uvuvi kwani katika mwongozo wa sera za uvuvi imetoa Mamlaka kwa jamii kushirikishwa.
"Serikali imefanya mahali pake, siyo kila mahali inaweza kufika, na kule ambapo sisi tumeweza kufika tunashirikiana na halmashauri za Mkinga, Jiji Tanga na wenzetu wa Muheza katika kuhakikisha kwamba tunasaidia utengenezaji wa mipango ya usimamizi wa rasilimali za uvuvi".
Amesema katika Wilaya ya Mkinga kwasasa wanatekeleza mpango wao uliopendekezwa na kukamilika wa mwaka jana ambapo moja ya mpango huo ulikuwa ni kupata ofisi na vifaa vya kisasa vya baharini ambayo vinawasaidia katika shuhuli za utafiti na matukio yasiyo endelevu baharini.
"Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita tulifanikiwa kushirikiana na serikali katika kumalizia ujenzi wa jengo la ofisi za wenzetu wa hifadhi za bahari ambalo tulianzia katikati, tukafanya ushiriki wetu na ilitugarimu kiasi cha shi Milioni 178, katika Kijiji cha Moa, wilayani Mkinga,
"Lakini sambamba na hilo wananchi wale pia walikuwa na pendekezo la kuongezea thamani mazao ya baharini, hivyo kuna vikundi vya wajasiriamali ambayo vimenufaika na wanasindika mazao ya mwani kutengeneza sharubati na unga, wengine biskuti na donati za samaki" ameongeza.
Social Plugin