Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATAKA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA KUWA ENDELEVU




Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya, huku ikijivunia mafanikio makubwa katika vita hiyo kupitia uwekezaji wa vifaa vya kisasa, usimamizi thabiti na operesheni zinazoongozwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Katika maadhimisho hayo ya kitaifa yaliyofanyika leo June 26,2025 jijini Dodoma, Waziri Mkuu wa JamhuriHayo ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Tanzania imeondolewa kwenye ramani ya kuwa kituo hatarishi cha dawa za kulevya, ikiwa ni matokeo ya kazi kubwa ya udhibiti iliyoimarishwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

“Katika kipindi cha miaka minne, zaidi ya tani milioni 4.8 za dawa za kulevya zimekamatwa nchini kupitia operesheni za ndani na za kimataifa. Tanzania sio mahali salama kwa watumiaji, wauzaji wala wasafirishaji wa dawa hizo,” amesema Majaliwa.

Amesema Rais Dk. Samia ameongeza bajeti kwa taasisi husika zikiwemo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ili kuhakikisha wanapata mitambo ya kisasa ya kufuatilia na kugundua dawa hizo kabla hazijaleta madhara.

Aidha, Majaliwa a.etumia jukwaa hilo kuwahimiza viongozi wa kisiasa kuendesha kampeni na siasa za kistaarabu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa mafanikio ya mapambano dhidi ya uhalifu.

“Tukivuruga amani, hakuna juhudi zitakazoendelea. Tuwe makini na kauli zetu, tuache uchochezi na matusi,” alionya.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, alimtunuku Rais Dk. Samia tuzo maalumu kwa mchango wake mkubwa katika mapambano hayo, akisema:

“Uwekezaji wake umeleta matokeo chanya,Vifaa vya kisasa vilivyopatikana kupitia bajeti aliyoidhinisha vimesaidia kubaini na kukamata dawa nyingi kwa muda mfupi.”ameeleza

Kamishna wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mwaka jana pekee walikamata kilogramu milioni 2.3 za dawa za kulevya, nyingi zikiwa zinajaribu kuingia kupitia Bahari ya Hindi.

A.esema mafanikio hayo ni sehemu ya jitihada za kimkakati zinazoendelea kuifanya Tanzania kuwa kinara wa udhibiti Afrika.

“Tutaendelea kufanya kazi usiku na mchana hadi tuuvunje kabisa mtandao huu haramu,” ameahidi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewashukuru wadau wanaoshiriki katika kupambana na janga hilo kwa kutoa taarifa, kuwaibua waraibu na kusaidia hatua za kisheria kuchukuliwa.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com