Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUVUMA YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA KWA MSISITIZO WA HAKI NA MAADILI

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Ngolo Malenya akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika katika halmashauri ya Wilaya ya Madaba akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas 

Na Regina Ndumbaro Madaba -Ruvuma 

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2025 katika Mkoa wa Ruvuma yamefanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, yakiongozwa na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Malenya, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed. 

Maadhimisho hayo yamebebwa na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tuendako”, ikiwa na lengo la kutoa hamasa kwa jamii kulinda na kutetea haki za watoto katika kila hatua ya maisha yao.

Katika tukio hilo muhimu, viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wamehudhuria akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Comrade Oddo Kilian Mwisho. 

Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa Mkoa wa Ruvuma una jumla ya watoto 855,106 wenye umri wa miaka 0-17, sawa na asilimia 46.3 ya watu wote 1,848,794. 

Kati yao, wavulana ni 428,058 na wasichana 427,048. Hali hii inaonesha wazi kuwa watoto ni kundi kubwa na lenye umuhimu mkubwa katika mustakabali wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Kupitia hotuba hiyo, Malenya amesisitiza umuhimu wa kila mdau katika jamii kuhakikisha watoto wanapata haki ya kuishi, kupata elimu, ulinzi na malezi bora. 

Aidha, amesisitizwa kuwa Serikali katika awamu zote imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kulinda amani na utulivu wa nchi, jambo ambalo ni urithi muhimu kwa watoto wetu. 

Wananchi wamehimizwa kuendeleza tunu hii adhimu kwa ajili ya ustawi wa taifa na kizazi kijacho.

Wazazi, walezi, jamii na wadau mbalimbali wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maadili mema kwa watoto, kuzuia unyanyasaji na kutumia lugha chanya kwa kuwa watoto hujifunza kwa kuiga. 

Malenya amehimiza jamii kuepuka lugha za kichochezi au vitendo vinavyoweza kuathiri malezi ya watoto na kuharibu mustakabali wao. 

Kauli mbiu ya mwaka huu imetumika kama kichocheo cha tafakuri na hatua madhubuti katika ulinzi wa haki za watoto wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com