
Mkuu wa mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko amewataka wakurugenzi wa halmashauri pamoja na wakuu wa wilaya mkoani hapa kuhakikisha Jamii inatumia vyakula vyenye virutubishi ili iweze kubadili hali ya udumavu pamoja na kutumia chakula bora.
Maagizo hayo ameyatoa leo Juni 10, 2025 katika kikao kazi kilichowakutanisha wadau wa chakula kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu urutubishaji wa chakula ambapo amewataka kuhakukisha jamii inapata uelewa juu ya urutubishaji wa chakula na kuondoa imani potofu kuhusu chakula kilichorutubishwa.
"Mkoa wetu bado unakabiliwa na changamoto ya udumavu ambapo kwa sasa umefikia 32% na kuna changamoto kuhusu uelewa wa virutubishi na lishe pamoja na Matumizi ya chakula kilichorutubishwa, hivyo jamii inahitaji elimu iweze kuona umuhimu wa kutumia chakula ambacho kimerutubishwa," amesema Mhe. Mrindoko.
Pamoja na kuwa mkoa wa katavi unatekeleza mkataba wa lishe wa Taifa uliosainiwa baina ya wakuu wa mikoa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan Septemba 30, 2022, mkoa wa Katavi unatekeleza mkataba wa ziada wa lishe kwa lengo la kuhakikisha unatokomeza tatizo la udumavu.
Kwa kuongeza kiini lishe kwenye chakula kutokana na kuwa mkoa wa Katavi unazalisha chakula kwa wingi pamoja na kuongeza virutubishi kwenye chakula kupitia mashine za usindikaji wa mazao ambapo leo mkoa wa Katavi umepokea mashine 20 kwaajili ya kazi hiyo ambapo kwa sasa mashine 15 za kusaga unga kati ya 359 zinaongeza virutubishi kwenye chakula sawa na 73%
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango mkakati wa wa kukabiliana na udumavu mkoani hapa katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji Nehemia James amesema Mkoa unaendelea na kampeni ya kukabiliana na udumavu na mpango harakishi na shirikishi wa kupunguza udumavu.
Aidha akitoa mafunzo ya uelewa wa umuhimu wa kurutubisha chakula Peter Kaja kutoka wizara ya Afya amesema Lengo ni kuboresha afya ya mlaji kwa nia ya kuzuia au kutibu matatizo ya kilishe yanayotokana upungufu wa virutubishi fulani muhimu mwilini, kama vile vitamini A, madini chuma, na madini joto.
Ameongeza kuwa sehemu kubwa ya jamii inakula vyakula vya nafaka zilizokobolewa au vyakula vya mizizi ambavyo kwa kawaida vina kiwango kidogo sana cha virutubishi kama vile madini chuma, vitamini A, na madini joto Ukoboaji hupoteza sehemu kubwa ya virutubishi kwani sehemu kubwa (75%) ya vitamini na madini zinazopatikana kwenye pumba na kiini.





Social Plugin