Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA ATOA POLE KUFUATIA AJALI YA KUSIKITISHA SAME – WATU 37 WAFARIKI DUNIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameungana na Watanzania kuomboleza vifo vya watu 37 waliopoteza maisha na wengine 30 kujeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea Juni 28, 2025 eneo la Sabasaba, barabara kuu ya Moshi – Tanga, katika wilaya ya Same, mkoa wa Kilimanjaro.

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Rais Samia ameandika:

"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya ndugu zetu 37 na majeruhi 30 kutokana na ajali ya barabarani iliyotokea jana jioni eneo la Sabasaba, Barabara Kuu ya Moshi - Tanga, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, kwa magari mawili kugongana na kuungua moto.


Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu marehemu wote wapumzike kwa amani, na majeruhi wote wapone kwa haraka. Ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Nurdin Babu, familia zote za wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki. Mwenyezi Mungu awape faraja na nguvu katika kipindi hiki kigumu.


Kama ambavyo nilieleza Juni 27 katika Hotuba yangu ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12, ajali za barabarani zimeendelea kugharimu maisha ya wapendwa wetu. Ninawasisitiza madereva kuendelea kuzingatia kwa umakini mkubwa sheria za usalama barabarani, na Jeshi la Polisi kuendelea kusimamia kikamilifu sheria hizo.”
 

Ajali hiyo imetokea majira ya jioni baada ya basi la Kampuni ya Channel One lenye namba za usajili T 179 CWL lililokuwa likitoka Moshi kuelekea Tanga, kugongana uso kwa uso na basi dogo aina ya Coaster lenye namba T 199 EFX lililokuwa likitoka wilayani Same. Gari zote mbili zilishika moto, na kusababisha vifo vya kusikitisha.
 
RC Kilimanjaro: “Ni Msiba Mkubwa Kwa Taifa”

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, amefika eneo la tukio na kuwajulia hali majeruhi hospitalini.

 Akizungumza na waandishi wa habari, amesema:

Mpaka sasa Watanzania 37 wamefariki, tunao majeruhi 29 ambapo 24 wapo hapa katika Hospitali ya Mji Same na wengine watano wamekimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi na KCMC. Kwa kweli ni msiba mkubwa,” amesema Mhe. Babu.

Aidha, alieleza kuwa serikali imeanza upimaji wa vinasaba (DNA) ili kusaidia utambuzi wa miili ya marehemu walioungua na kutotambulika kwa macho.


"Tunaomba wananchi wote wanaohisi ndugu zao hawajulikani walipo wafuatilie taarifa hizi ili kusaidia utambuzi wa miili iliyobaki,” ameongeza RC Babu.
 
CHANZO CHA AJALI: Tairi Kupasuka

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la mbele la basi la Channel One, hali iliyosababisha dereva kupoteza mwelekeo na kugongana uso kwa uso na Coaster kabla ya magari hayo kuwaka moto.

Uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea huku wananchi wakihimizwa kuwa watulivu na kufuatilia taarifa kutoka mamlaka husika.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com