Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANI 30 ZA PAMBA ZILIZOPIMWA KINYUME NA TARATIBU ZAZUIWA KISHAPU..DC AONYA KUPUNJA WAKULIMA

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza na wananchi wa Ngofila wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ununuzi wa pamba katika vyama vya msingi na kufanya mkutano wa hadhara Ngofila lengo ikiwa ni kufuatilia mafanikio na changamoto za msimu wa ununuzi wa pamba ili kuhakikisha mnyororo wa masoko unakwenda vizuri bila kukwamishwa na ukiukwaji wa taratibu Juni 3,2025

Na Sumai Salum – Kishapu

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi ameagiza kampuni ya Aham Limited kushusha tani 30 za pamba zilizonunuliwa kinyume na taratibu kutoka Chama cha Msingi cha Kiloleli (Amcos), akisisitiza kuwa ununuzi huo ulifanyika kwa kutumia mizani isiyo rasmi na hivyo kukiuka kanuni za ununuzi wa zao hilo.

Akizungumza Juni 3,2025, wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ununuzi wa pamba katika vyama vya msingi vya Mwamashele, Mwamanota, Inolelo (Amcos ya Raha ya Balimi), Ngofila, Kalitu na Kiloleli na kufanya mkutano wa hadhara Ngofila, Mhe. Masindi amesema lengo ni kufuatilia mafanikio na changamoto za msimu wa ununuzi wa pamba ili kuhakikisha mnyororo wa masoko unakwenda vizuri bila kukwamishwa na ukiukwaji wa taratibu.

"Aham amenunua pamba kupitia mzani ya kawaida badala ya mzani wa kidijitali kama inavyotakiwa, kuanzia sasa naagiza pamba yote ishushwe na ipimwe upya kwa kutumia mzani wa kidijitali ili kuwezesha serikali kupata mapato stahiki na taarifa sahihi kwa Bodi ya Pamba," amesema Masindi.

Ameeleza kuwa matumizi ya mizani isiyo rasmi yanapotosha takwimu muhimu kwa Halmashauri, husababisha kukosekana kwa makadirio sahihi ya ushuru wa 3% kwa kilo moja, na hata kuathiri taarifa za idadi ya wakulima husika jambo ambalo ni muhimu kwa maandalizi ya msimu ujao kwa bodi ya pamba vilevile, ameonya kuwa mkulima huenda akapunjwa, huku mnunuzi akijikuta akikumbwa na adhabu za kusafirisha mazao bila vibali halali.

Katika hatua nyingine, kufuatia malalamiko kutoka kwa wakulima wa Kata ya Ngofila kuhusu kucheleweshwa kwa malipo Masindi amemuelekeza mnunuzi kutoka Lugeye Company Limited anayenunua pamba katika vyama vya msingi vya Mwamanota, Ngofila na Kalitu kuhakikisha anawalipa wakulima wote kwa wakati.

"Mpango wa serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha mkulima ananufaika hivyo kama mnunuzi hana fedha za kulipa, apishe mnunuzi mwingine hatutaki ucheleweshaji wa malipo wala ubadhirifu wowote kwenye mizani na wote wanaonunua pamba kwenye maeneo husika waende kwa wakati kama kuna sababu nyingine watueleze mapema ili turuhusu wanunuzi wengine kuendelea na ununuzi pamba" amepngeza kwa msisitizo.

Mkuu huyo wa Wilaya pia amewasihi wakulima kuuza pamba kwenye vyama vya msingi pekee huku wakijiwekea mipango ya muda mfupi, kati na mrefu kwa ajili ya kuboresha maisha yao kupitia zao la pamba akiwakumbusha umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya watoto wao,kuweka akiba ya fedha na vyakula, ujenzi wa nyumba bora na uzingatiaji wa lishe bora kutokana na fedha watakazozipata.

"Mwanaume aliyefanikiwa huwa na mwanamke nyuma yake hivyo msitumie fedha za pamba kwa 'nzige' (wanawake wauzao miili yao) watamaliza fedha zenu na kuwaachia magonjwa, mwisho wake mtawatesa wake na watoto wenu",ameongeza.

Masindi ameeleza kuridhishwa na mwenendo wa ukusanyaji wa pamba huku akihimiza wakulima kuuza pamba safi ili wapate bei nzuri na kuhakikisha vyama vya msingi vinafuata maelekezo ya serikali na Bodi ya Pamba katika ununuzi na uuzaji.

Malunde 1 Blog imemtafuta Mwakilishi wa Kampuni ya ununzi wa pamba ya Lugeye, Juni Butina ili kupata majibu ya ucheleweshwaji malipo kwa wakulima, ambapo amesema changamoto iliyotokea ni ucheleweshwaji wa taarifa ya kuomba fedha kutoka kwa viongozi wa Amcos ili waletewe kwa wakati lakini kampuni hiyo itahakikisha inafuata taratibu zote za ununuzi walizoelekezwa na serikali ya Wilaya na bodi ya pamba.

Takwimu za Ukusanyaji Pamba (Hadi Juni 3, 2025)

Mwamashele Amcos Tani 7 Mnunuzi ni Bioustain Tanzania Ltd,Mwamanota Amcos Tani 12,Inolelo (Raha ya Balimi) Tani 14,Ngofila & Kalitu Amcos zaidi ya Tani 10Mnunuzi ni Lugeye Company Ltd pamoja   Kiloleli Amcos zaidi ya Tani 50 na Mnunuzi ni Aham Company Limited.

Mnamo mwezi Mei,15,2025 Mkuu wa Wilaya ya Kishapu alizindua msimu mpya wa pamba 2025/2026 kwa ngazi ya Wilaya akikutana na wadau mbalimbali wa zao hilo ambapo masuala muhimu yalizungumziwa kuhusu bei,mizani,ubora wa pamba,uuzaji na ununuzi ambapo pamba safi itauzwa kwa bei elekezi ya Tsh. 1,150 kwa kilo, huku pamba fifi ikiuzwa kwa Tsh. 575 kwa kilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza na Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha ushirika (Amcos) Raha ya Balimi Inolelo Kanogu Luzwilo kuhusiana na mwenedo wa ununuzi wa pamba msimu wa 2025/2026 kwenye ziara yake yenye lengo ni kufuatilia mafanikio na changamoto za msimu wa ununuzi wa pamba ili kuhakikisha mnyororo wa masoko unakwenda vizuri bila kukwamishwa na ukiukwaji wa taratibu Juni 3,2025
Afisa Tawala wa Kishapu Mkoani Shinyanga Fadhiri Mvanga akizungumza kwenye ziara ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Peter Masindi ya ukaguzi wa ununuzi wa pamba katika vyama vya msingi na kufanya mkutano hadhara ikiwa lengo ni kufuatilia mafanikio na changamoto za msimu wa ununuzi wa pamba ili kuhakikisha mnyororo wa masoko unakwenda vizuri bila kukwamishwa na ukiukwaji wa taratibu Juni 3,2025.
Mkaguzi wa pamba Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga kutoka bodi ya pamba Catherine Anthony akizungumzia sheria za bodi hiyo kwa wakulima,vyama vya msingi na makampuni ya ununuzi wa pamba kwenye ziara ya Mkuu wa Wilaya hiyo ya ukaguzi wa ununuzi wa pamba katika vyama vya msingi na kufanya mkutano wa hadhara ikiwa lengo ni kufuatilia mafanikio na changamoto za msimu wa ununuzi wa pamba ili kuhakikisha mnyororo wa masoko unakwenda vizuri bila kukwamishwa na ukiukwaji wa taratibu Juni 3,2025
Mkuu wa divishen ya kilimo,mifugo na ushirika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mwita Mwijarubi akizungumza kwenye ziara ya Mkuu wa Wilaya hiyo ya ukaguzi wa ununuzi wa pamba katika vyama vya msingi na kufanya mkutano wa hadhara lengo ikiwa ni kufuatilia mafanikio na changamoto za msimu wa ununuzi wa pamba ili kuhakikisha mnyororo wa masoko unakwenda vizuri bila kukwamishwa na ukiukwaji wa taratibu Juni 3,2025
Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha ushirika (Amcos) Ngofila Mariam Steven akiwasilisha malalmiko ya wananchi na chama cha msingi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi kuhusiana na hali ya uuzaji na ununuzi zao la pamba kwa mwekezaji wa eneo hilo Lugeye Company Limited Juni,3,2025 kwenye mkutano wa hadhara wa mkuu huyo
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.Peter masindi akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ngofila Wilayani humo Juni 3,2025
Mwakilishi wa kampuni ya Lugeye Juni Bitana akizungumzia tuhuma za ucheleweshaji malipo kwa wakulima wa pamba Kata ya Ngofila Wilayani Kishapu Mkoani Shinyinga Juni 3,2025 baada ya wakulima kulalamika mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Peter Masindi kwenye ziara yake ya ufuatiliaji maendeleo ya ununuzi wa pamba Juni 3,2025 
Pamba tani 30 iliyonunuliwa na kampuni la Aham kwenye chama cha msingi cha ushirika (Amcos) Kiloleli wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Peter Masindi ameagiza ishushwe na ipimwe upywa kutumia mzani wa digital Juni,3,2025
Afisa ushirika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkaoni Shinyanga Isack Shoo
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.Peter Masindi (Kulia) na Katibu msaidizi wa Amcos ya Kiloleli Daniel Dogani(kushoto)

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe.Peter Masindi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwamanota

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com