Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIGOGORO YA ARDHI VIJIJI VINAVYOZUNGUKA MIGODI KISHAPU KUKOMESHWA


Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Tume ya Mipango ya Ardhi Bw. Amos Mpuga akizungumzia ukamilishaji zoezi la kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi hatua ya 1-4 Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga katika Vijiji Kumi na sita (16) vinavyozunguka maeneo ya migodi ya Williamson na Al hilal Juni 26,2025

Na Sumia Salum-Kishapu

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini imekamilisha zoezi la kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga katika Vijiji Kumi na sita (16) vinavyozunguka maeneo ya migodi ya Williamson na Al hilal.

Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa Tume hiyo Bw.Amos Mpuga akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo na Mkurugenzi Mtendaji amesema zoezi hilo lililenga Vijiji 16 na vyote vimefikiwa ikiwa ni utekelezaaji wa maelekezo ya Kamati ya Mawaziri ya kufanya tathimini ya maeneo yenye migogoro iliyoundwa chini ya Hayati Mhe.Rais Dkt John Pombe Magufuri.

"Kwa Wilaya ya Kishapu ilibainika kuwa maeneo yenye migogoro ni Vijiji vinavyopakana na migodi ya madini kwani vipo baadhi ya vijiji vilikuwa vimeingilia mipaka ya maeneo ya migodi na vingine vinavyozunguka vilikuwa vinaendelea kuingilia migodi, hivyo mapendekezo ya Mawaziri yalikuwa Vijiji vilivyovamia kwa kiwango kikubwa maeneo ya migodi waachiwe maeneo hayo wananchi na maeneo ambayo hayajavamiwa na wananchi yalindwe kwa ajili ya migodi" amesema Mpuga.

Mpuga ameongeza kuwa baada ya serikali kubaini hivyo Kamati ilitoa maelekezo ya uandaaaji wa mipango wa matumizi ya ardhi ili kuondoa migogoro inayosababishwa na wananchi kuvamia maeneo ya migodi.

"Kipekee nikushukuru Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kwa kutupa ushirikiano kwani tumefaanikiwa kwa kiwango kikubwa ukamilishaji wa zoezi hili ndani muda uliopangwa,tumekamilisha hatua ya kwanza hadi ya nne kwa kutenga maeneo ya matumizi mbalimbali ikiwemo Kilimo,Malisho,uchimbaji mdogo na mengine yaliyopendekezwa na wananchi kulingana na uhitaji wao na Vijiji vyote wameunda sheria ndogo ya kulinda maeneo yaliyotengwa kwa matumizi husika"Ameongeza.

Amesema zimebakia hatua mbili ikiwa ni hatua ya Mipango Kina na utoaji Hati Milki kwenye maeneo hayo ili yawe na tija kwa wananchi lengo likiwa ni kuondoa migogoro na wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia ardhi waliyonayo.

"Kama eneo limetengwa kwa ajili ya kilimo hivyo ni wajibu wa Maafisa kilimo kuwaelimisha kuhusiana na kilimo bora na cha kisasa ili wananchi wazalishe kwa kiwango kikubwa na wajipatie kipato na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya migodi wataalamu wake pia watatoa elimu ya kina ili wachimbaji wetu wadogowadogo wachimbe kwa tija na kujikwamua kiuchumi vivyo hivyo na maeneo mengine wataalamu husika watatoa elimu ya kina" Ameongeza Mpuga

Amesema baada ya hayo maeneo kufanyiwa mpango kina kila mwananchi atapewa hati milki kwa ajili ya kumiliki rasmi maeneo yao kwani hadi sasa bado wanayamiliki kienyeji hivyo usalama wake bado ni mdogo ni rahisi mtu kudhurumiwa ama kunyang'anywa eneo lake ambalo halina hati ila eneo lililopimwa na kuwa na hati linakuwa na ulinzi wa kisheria.

Ametoa rai kwa serikali ya Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwa na utaratibu wa kutenga bajeti za ukamilishaji hatu zilizobakia na Tume itasaaidia kujenga uwezo kwa timu ya Mipango ya matumzi ya ardhi ya Wilaya ili waendelee na mchakato wa upimaji na utoaji wa hati milki kwenye meneo ya wananchi.

Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.Peter Masindi amepongeza jitihada za serikali za kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kuimarishwa kwa wananchi kwani baada ya hatua zote kukamilika hakutakuwa na migogoro ambayo imekuwa ikisababisha baadhi ya maisha ya watu kuwa hatarini na wengine kupoteza maisha kwa kugombania ardhi.

"Zoezi hili likikamilika kila mwananchi atajua mipaka yake na hakuna atakayeweza kumuingilia mwingine maana kila ardhi itatambulika kisheria tofauti na umilki wa kienyeji ambao watu uweka mawe ama kupanda KataniMpaka ambavyo kiuhalisia vinamishika, hivyo niiombe Tume tena endapo mtapata fedha mtusaidie kwenye Vijiji vingine vilivyobakia hata visivyo zunguka migodi kwani migogoro ya ardhi bado ni kitendawili kwa baadhi ya maeneo"Amesema Mkuu huyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Emmanuel Johnson amekiri kuwepo kwa migogoro kwenye Vijiji 16 vinavyozunguka migodi hiyo hivyo kutokana na ushirikishwaji wananchi katika mpango huo umesaidia kuwaelimisha na kuwapa imani Halmashauri ya uwepo wa utatuzi wa kudumu wa migogoro ya ardhi kwenye maeneo hayo kwani wawekezaji na wananchi watakuwa salama kila mmoja kwenye eneo lake.

Johnson amesema lengo la Halmashauri ni kufikia Vijiji vyote kwa kutengenezewa mpango wa matumizi bora ya ardhi huku akiahidi Halmashauri itatenga fedha kupitia mapato ya ndani,Csr na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Vijiji vyote vinafikiwa na mpango huo.

'Tunatamani kuona mpango huu ukifikia mwisho tunaamini tutapata faida kubwa katika Wilaya yetu mapato yataongezeka kwa sababu pindi tu ukamilikashwaji ugawaji Hati Milki ukikamilika wananchi watapata mikopo na kufanya biashara na uwekezaji mbalimbali watajikwamua kiuchumi na watalipa kodi ya serikali pia"Amesema Johnson.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.Peter Masindi akizungumza na watumishi wa Kanda ya Kaskazini wa Tume ya Mipango ya Ardhi baada ya ukamilishaji hatua ya 1-4 zoezi la kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi Wilayani humo katika Vijiji Kumi na sita (16) vinavyozunguka maeneo ya migodi ya Williamson na Al hilal Juni 26,2025

Mkurugenzi Mtendaji Halmashuri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson akizungumza na watumishi wa Kanda ya Kaskazini wa Tume ya Mipango ya Ardhi baada ya ukamilishaji hatua ya 1-4 zoezi la kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi Wilayani humo katika Vijiji Kumi na sita (16) vinavyozunguka maeneo ya migodi ya Williamson na Al hilal Juni 26,2025

Mratibu wa timu ya mipango ya ardhi na Afisa ardhi wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Grace Pius







Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.Peter Masindi (wa tatu kutoka kulia),Maafisa wa Tume ya Mipango na Matumizi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini na Afisa ardhi wa Halmashauri hiyoJuni 26,2025

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson (aliyekaa),Maafisa wa Tume ya Mipango na Matumizi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini na Afisa ardhi wa Halmashauri hiyo Juni 26,2025

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com