Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHENGERWA APIGA MARUFUKU UHAMISHAJI FEDHA ZA MIRADI :"TUTAVUNJA MIKATABA KWA WAKANDARASI GOIGOI




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amepiga marufuku tabia ya baadhi ya makandarasi kuhamisha fedha walizolipwa na serikali kwa ajili ya miradi maalum na kuzitumia kwenye shughuli nyingine tofauti.

Akizungumza jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya miji kupitia Mpango wa TACTIC, Mchengerwa amesema serikali haiwezi kuvumilia uzembe na uvunjaji wa masharti ya mkataba unaofanywa na baadhi ya wakandarasi.

“Kumekuwepo na tabia isiyokubalika ya baadhi ya makandarasi kuhamisha fedha walizolipwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuzitumia katika maeneo mengine. Hii inasababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi licha ya serikali kuwa imeshatoa malipo yote,” amesisitiza Waziri Mchengerwa.

Ameagiza kuwa mkandarasi yeyote atakayebainika kufanya hivyo achukuliwe hatua kali ikiwemo kuvunjiwa mkataba wake mara moja. Alisisitiza kuwa viongozi wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri pamoja na wataalam wa TARURA wanapaswa kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa miradi hiyo.

"Wekeni utaratibu wa kusimamia kwa karibu. Mkandarasi akionekana hana uwezo au anakiuka masharti ya mkataba, vunjeni mkataba na kumpa aliye tayari na mwenye uwezo," amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo aliagiza kuwa makandarasi wote waliotia saini mikataba hiyo kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati, vinginevyo watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutiwa kazi.

“Hakuna sababu ya kuchelewesha miradi wakati fedha zote zimeshalipwa. Wananchi wanahitaji huduma, hatuwezi kuendelea kuwavumilia wanaotuchelewesha,” aliongeza.

Aidha, Mchengerwa ameelekeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo uzingatie ushirikishwaji wa wananchi waliopo kwenye maeneo husika, hasa kwa kuwapa ajira na fursa za kiuchumi katika maeneo yao.

Kwa upande mwingine, alizitaka halmashauri zenye miradi ya ujenzi wa masoko kuhakikisha kuwa mara baada ya kukamilika, masoko hayo yawe na uwezo wa kujiendesha yenyewe kwa ufanisi.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Rogatus Mativila, alieleza kuwa mikataba iliyosainiwa ni 13, inayolenga kutekelezwa kwenye miji 11, ikiwa na thamani ya Dola za Kimarekani milioni 410, sawa na takriban Shilingi trilioni 1.1.

“Mikataba hiyo inahusisha ujenzi wa masoko, stendi za mabasi, barabara pamoja na ufungaji wa taa katika mitaa ya miji husika,” amefafanua Mativila.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com