Baadhi ya wakulima na viongozi wa Mapendo Amcos wakiangalia miti ya kahawa iliyostawi vizuri
Na Regina Ndumbaro Nyasa-Ruvuma
Wakulima wa kahawa katika kijiji cha Mpepo, Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wameipongeza Serikali kwa kuwapatia mbolea za ruzuku zilizosaidia kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama za uzalishaji wa zao hilo.
Ilbert Mahai, mmoja wa wakulima wa kijiji hicho, amesema kuwa tangu aanze kupokea mbolea hiyo, uzalishaji wa kahawa umeongezeka kutoka tani 20 mwaka 2022/2023 hadi kufikia tani 150 msimu wa 2024/2025, huku akitarajia kuvuna tani 200 katika msimu ujao.
Aidha, wakulima wameeleza kuwa ruzuku hiyo imewawezesha kuajiri nguvu kazi zaidi, jambo ambalo limechochea ajira hasa kwa vijana na wanawake wa vijiji vya Mpepo, Ndondo na Mtetema.
Alto Matembo mkulima wa kijiji cha Ndondo amesema kupitia kilimo cha kahawa ameweza kujenga nyumba bora na kusomesha watoto hadi chuo kikuu, akisisitiza umuhimu wa kujiunga na vyama vya ushirika kama Mapendo Amcos kwa ajili ya kupata soko la uhakika.
Serikali pia imepongezwa kwa kuanzisha mradi wa kuzalisha miche bora ya kahawa aina ya Kombat katika kijiji cha Mpepo, hatua ambayo imewasaidia wakulima kuepuka gharama kubwa za kununua miche kutoka Mbinga.
Method Ngonyani kutoka Mtetema amesema kuwa upatikanaji wa miche hiyo ni bure kupitia Halmashauri na Bodi ya Kahawa Tanzania umewahamasisha wengi kuachana na mazao yasiyo na tija kama mahindi na kuhamia kwenye kahawa.
Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika Mapendo, Panglas Komba, amesema wamefanikiwa kununua mtambo wa kuchakata kahawa wenye uwezo wa kuhudumia wakulima 200 kwa wakati mmoja, hatua iliyoboreshwa ubora wa kahawa.
Hata hivyo, ameiomba Serikali kuwasaidia mashine kubwa zaidi kutokana na mahitaji makubwa kutoka kwa wakulima, huku akihimiza wakulima kuacha kuchakata kahawa majumbani ili kuboresha ubora na thamani ya mazao yao.
Social Plugin