Na Mwandishi Wetu Mbinga-Ruvuma
Halmashauri ya wilaya ya mbinga mkoani Ruvuma imeweka historia ya kiutendaji kwa kufanikisha ukusanyaji wa Shilingi bilioni 12.2 dhidi ya lengo la awali la Shilingi bilioni 8.4, hadi kufikia tarehe 30 Juni 2025.
Akizungumza katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), mkuu wa kitengo cha fedha na uhasibu CPA Samwel Marwa amesema kuwa mapato ya halmashauri hiyo yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 3.4 mwaka 2021 hadi bilioni 12.4 mwaka 2025.
CPA Marwa amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri baina ya wataalamu wa Halmashauri, madiwani, na wananchi kwa ujumla.
Ameeleza kuwa uzingatiaji wa sheria ndogo za Halmashauri na usimamizi thabiti katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato, umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo.
Ametaja vyanzo vikuu vya mapato kuwa ni ushuru wa zao la kahawa (Sh. bilioni 4.3), makaa ya mawe (Sh. bilioni 3.3), ushuru wa huduma (Sh. bilioni 1.35), ushuru wa mahindi, na michango kutoka kwa wananchi ngazi ya kata.
Katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa magari kwa ajili ya ukusanyaji mapato, halmashauri imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kutumia magari yaliyopo kwa zamu na kuanzisha kituo maalum cha ukaguzi wa magari yanayobeba makaa ya mawe katika eneo la Lipokela.
Halmashauri pia imeendelea kushirikiana na taasisi kama tume ya madini katika kuhakikisha mapato yote yanayopaswa kukusanywa hayaishii mikononi mwa walaghai.
Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Mary Makondo, ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ikiwa ni mwaka wa nne mfululizo.
Amesisitiza kuwa kupata hati safi ni kielelezo cha usimamizi bora wa fedha na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia sheria na miongozo ya Serikali.
Makondo amesisitiza matumizi ya mfumo wa kisasa wa ukusanyaji mapato wa TAUSI na kutaka usimamizi wa karibu katika majibu ya hoja za CAG na maagizo ya LAAC.
Kwa upande wake, mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali mkoa wa Ruvuma, Nicolas Kilinga, amesisitiza umuhimu wa halmashauri kujibu hoja zote za ukaguzi kwa wakati ili kuzuia ongezeko la hoja mpya.
Social Plugin