Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KIONGOZI WA JUMUIYA YA WAZAZI CCM MASASI AFARIKI DUNIA

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika msiba wa aliyekuwa katibu na diwani wa kata ya Namwanga wilayani Masasi Mkoani Mtwara

Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara

Mjumbe wa Baraza la Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Masasi, Ndugu Edwin Stevin Kasembe, ameaga dunia ghafla katika nyumba yake, mtaa wa Masasi Mbovu, Masasi Mjini.

Kasembe, ambaye pia aliwahi kuwa Diwani mstaafu wa Kata ya Namwanga, amefariki akiwa nyumbani kwake, na kifo chake kimeacha simanzi kubwa kwa familia, jamii na viongozi wa CCM.

Mazishi ya Ndugu Kasembe yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa serikali, ambapo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Masasi, Bi. Mariam Kasembe, ameelezea kwa huzuni na kusema kuwa chama kimepoteza kiongozi muhimu.

Amewataka wanachama wa CCM kuungana na familia katika kipindi hiki cha maombolezo, na kushikamana katika kuhakikisha utamaduni wa chama unaendelea.

Katika ibada ya mazishi, kiongozi wa dini kutoka dhehebu la Kikristo, Kanisa Anglikana Mkuti Masasi, amesisitiza umuhimu wa kuishi maisha ya kumtegemea Mungu.

Amewaasa waombolezaji kuendelea kumtumikia Mungu na kuishi kwa upendo, licha ya huzuni inayowakumba.

Ndugu Edwin Stevin Kasembe amezikwa katika Makaburi ya Migongo Misheni, Masasi Mjini, ambapo jamii na viongozi wa dini wamekamilisha shughuli za mazishi kwa sala na maombi.

Kifo cha Kasembe kimeacha pengo kubwa katika jamii na CCM Masasi, na kitasalia kuwa kumbukumbu muhimu kwa wengi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com