Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha la michezo na burudani la Grand Bunge Bonanza linalotarajiwa kufanyika Jumamosi, Juni 21, 2025, katika viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlini, Miyuji jijini Dodoma.
Tamasha hilo litakutanisha wabunge, watumishi wa Bunge, taasisi za Serikali na wananchi kwa ujumla, likiwa ni la mwisho kufanyika katika Bunge la Kumi na Mbili.
Bonanza hilo pia limelenga kuimarisha afya, mshikamano na mahusiano baina ya Bunge na wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa maandalizi ya Bonanza hilo, Festo Sanga, amesema tamasha hilo litabeba kaulimbiu isemayo “Shiriki Uchaguzi Mkuu, kwa Maendeleo ya Taifa Letu” ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi kwenye demokrasia ya nchi.
Sanga amesema michezo ya ushindani itakayofanyika ni pamoja na mpira wa miguu kati ya Bunge na CRDB, mpira wa pete kati ya Bunge na PSSF, kuvuta kamba kwa wanaume kati ya Bunge na Wizara ya Maliasili na Utalii, na kwa wanawake kati ya Bunge na Wizara ya Uchukuzi.
Aidha, mpira wa kikapu utachezwa kati ya Bunge na BOT kwa wanaume na kati ya Bunge na CRDB kwa wanawake, huku mpira wa wavu ukichezwa kati ya Bunge na NSSF. Bunge pia litachuana na UDOM katika mpira wa kikapu kwa wanawake.
Mbali na michezo hiyo, kutakuwa na burudani mbalimbali na michezo ya kujifurahisha ikiwemo mpira wa meza, pool table, kucheza bao na drafti, kurusha tufe, darts, kukimbia na magunia, kufukuza kuku, kujaza maji kwenye chupa kwa kikombe, kushindana kunywa soda, kula chakula kwa kasi na kuvaa soksi kwa haraka.
Sanga ameeleza kuwa Benki ya CRDB, ambayo ni mdhamini mkuu wa Bonanza hilo, imetoa vifaa vyote vya michezo vikiwemo jezi, medali, tracksuit, mipira, fulana na kofia kwa washiriki wote. Aidha, CRDB imeandaa kifungua kinywa na tafrija ya jioni yenye burudani mbalimbali kama muziki wa dansi, taarabu, ngoma za asili, ushairi na vichekesho kutoka kwa wasanii wa stand-up comedy.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa CRDB, Bi. Tully Mwambapa, amesema benki hiyo imekuwa na ushirikiano wa karibu na Bunge katika kudhamini matukio ya kijamii na michezo, na mwaka huu Bonanza hilo limeandaliwa kwa mtindo wa kipekee unaolenga kuwaleta pamoja Watanzania katika hali ya burudani, michezo na mshikamano wa kitaifa.
Mwambapa amewahamasisha wakazi wa Dodoma na maeneo jirani kushiriki kwa wingi katika tukio hilo, akisisitiza kuwa ni fursa ya kipekee ya kuburudika na kujenga afya kwa pamoja.
Social Plugin