Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Katika hatua kubwa ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kuchochea ukuaji wa biashara bunifu nchini, Mradi wa Ubunifu wa FUNGUO umetangaza fursa mbili mpya za ufadhili zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya kusaidia wajasiriamali wa Tanzania – hususan wale wanaoendesha biashara endelevu kwa mazingira.
Fursa hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam Juni 27, 2025, na kuambatana na wito maalum kwa vijana na wanawake nchini kuhakikisha wanachangamkia fursa hizo ambazo zimeelezwa kuwa za aina yake katika kuchochea ajira, ubunifu na utunzaji wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa fursa hizo, Karina Dzialowska, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Utawala wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, amesema kuwa FUNGUO limekuwa daraja la matumaini kwa wajasiriamali wachanga na wadogo kote nchini.
“Kilichoanza kama mradi wa majaribio miaka minne iliyopita, sasa ni mhimili wa mfumo wa Tanzania wa kusaidia biashara changa. FUNGUO si tu linatoa fedha, bali linajenga uwezo na kuwaunganisha vijana na wanawake na masoko ya ndani na nje,” alisema Dzialowska huku akisisitiza kuwa asilimia 40 ya ruzuku hizo zimekusudiwa kwa wanawake.
Aidha, alitoa wito mahsusi kwa wanawake na vijana walioko mijini na vijijini kuwa na uthubutu wa kuwasilisha maombi ya ufadhili huo, akisisitiza kuwa hakuna ndoto ndogo iwapo kuna mpango madhubuti na dhamira ya kweli.
Kwa upande wake, William Nambiza, Mratibu wa Ushirikiano wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Finland nchini, alieleza kuwa kupitia mpango maalum wa #GreenCatalyst, serikali ya Finland inalenga kuchochea ubunifu wa ndani katika sekta ya misitu na uhifadhi wa mazingira.
“Tunahitaji ajira ambazo si tu zinaongeza kipato, bali pia zinalinda mazingira yetu. Biashara zinazojikita katika matumizi bora ya rasilimali na kuongeza thamani ya mazao ya misitu zinahitaji kupewa msukumo mpya,” alisema Nambiza, akiwasihi wajasiriamali wengi zaidi kuwasilisha maombi kupitia dirisha la mpango huo.
Naye John Rutere, Naibu Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania), alisisitiza kuwa FUNGUO si mradi wa kawaida, bali ni “safari ya kujenga kizazi cha biashara zinazotatua changamoto halisi.”
“Tunaangalia mbali zaidi ya faida binafsi. Tunataka kuona biashara zinazobadili maisha ya watu, zinazoajiri, na zinazolinda mazingira yetu. Hadi sasa, ajira zaidi ya 5,000 zimezalishwa kupitia FUNGUO, na zaidi ya TZS bilioni 15 zimekusanywa kama uwekezaji wa nyongeza kutokana na mitaji tuliyowekeza,” alisema Rutere.
Mradi wa FUNGUO unatekelezwa na UNDP kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya, Finland na Uingereza (kupitia FCDO), ukilenga kusaidia biashara ndogo, ndogo sana na za kati (MSMEs) katika sekta mbalimbali.
Fursa hizi mpya ni sehemu ya azma ya kujenga uchumi jumuishi unaojali mazingira, ubunifu na usawa wa kijinsia. Dirisha la maombi kwa ufadhili huo lipo wazi, na wajasiriamali kutoka mikoa yote ya Tanzania wanakaribishwa kuwasilisha maombi yao kupitia tovuti rasmi ya FUNGUO.
Social Plugin