

Katika hatua ya kuimarisha huduma za afya wilayani Nanyumbu, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara Mheshimiwa Christopher Edward Magala, amekabidhi rasmi gari la wagonjwa kwa kituo cha Afya cha Mikangaula.
Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya kituo hicho, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi wa kata ya Mikangaula.
Katika hafla hiyo, Mh. Magala amesomewa taarifa ya kituo hicho inayoonyesha mafanikio pamoja na changamoto zinazoikabili, ikiwemo uhaba wa watumishi wa afya.
Akijibu changamoto hiyo, Mh. Magala amewahimiza wazazi na jamii kwa ujumla kuwahamasisha watoto wao kusoma masomo ya sayansi ili waweze kuwa wataalamu wa baadaye na kusaidia kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi wa afya katika maeneo ya vijijini.
Aidha, Mh. Magala amewataka watumishi wa kituo cha afya Mikangaula kuhakikisha gari hilo linatumika kwa huduma za afya pekee kama lilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Nanyumbu, Dkt. Marco Mazanzagar, ametoa shukrani kwa serikali kwa msaada huo muhimu.
Amesema kuwa upatikanaji wa gari hilo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto za usafiri kwa wagonjwa, hasa wale wanaohitaji rufaa kwenda hospitali za wilaya au mkoa.
Wakazi wa kata ya Mikangaula nao wameonesha furaha yao, wakisema kuwa kupatikana kwa gari la wagonjwa ni hatua kubwa ya ukombozi kwao.
Wamesema kuwa hapo awali walikuwa wakikumbwa na changamoto kubwa ya usafiri wakati wa dharura, lakini sasa huduma zitafika kwa haraka na kuokoa maisha ya wengi.
Social Plugin