
Na ReginaNdumbaro- Masasi
Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mheshimiwa Rachel Kasanda, ameongoza zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika maeneo mbalimbali ya mji wa Masasi, lenye lengo la kuzoa taka pembezoni mwa barabara na maeneo ya biashara mfano madukani.
Zoezi hilo limefanyika kwa ushirikiano wa wananchi na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, ambao wamejitokeza kwa wingi kumuunga mkono kiongozi huyo.
Usafishaji huo ulifanyika kwa saa tatu, kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 mchana, ambapo taka zote zilikusanywa na kuondolewa kwa kutumia gari maalum na kutupwa nje ya mji kwenye dampo rasmi.
Zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa, likilenga kuimarisha afya ya jamii kwa kuondoa uchafu unaoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko mfano kipindupindu.
Wakazi wa Masasi wamempongeza Mkuu wa Wilaya kwa kujitolea kushiriki bega kwa bega katika kufanya usafi huo.
Walisema kitendo hicho ni cha kupigiwa mfano, na wamemtaka Mheshimiwa DC kuhakikisha zoezi hilo linafanyika mara kwa mara ili kuifanya Masasi kuwa jiji safi na lenye afya kwa muda wote.
Mara baada ya kumaliza kufanya usafi huo, Mheshimiwa Kasanda aliwashukuru wananchi wote waliojitokeza na kuwataka kuendelea kutoa ushirikiano katika kuboresha usafi wa mazingira.
Alisisitiza kuwa usafi si jukumu la mtu mmoja, bali ni jukumu la kila mwananchi, akimalizia kwa kusema, “Usafi ni Afya.”
Social Plugin