Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHAMA CHA MADAKTARI BINGWA WA UPASUAJI CHATOA WITO WA MABORESHO YA HUDUMA ZA AFYA NCHINI


Na Hadija Bagasha - Tanga

Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji nchini kimeishauri serikali kuimarisha huduma za upasuaji katika hospitali za wilaya kwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa na vya kutosha kuwaondolea wananchi usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Rais wa chama hicho, Dkt. Amani Malima, alisisitiza umuhimu wa serikali kuongeza uwekezaji katika vifaa na teknolojia za upasuaji kwa hospitali za wilaya.

Akizungumza kwenye mkutano huo Dkt Malima alisema  huduma za upasuaji bado zimekuwa na changamoto katika ngazi ya hospitali za wilaya, hali inayosababisha baadhi ya wagonjwa kuchelewa kupata matibabu kwa wakati.

“Kadri tunavyoenda tumeona hospitali za kimkoa zinafanya kazi za kikanda kwa hiyo sasa tunachotaka serikali za mikoa ziendelee kupeleka huduma za upasuaji kwenye kwenye hospitali za wilaya,sasa kadri unavyoshufha chini ndio unavyoboresha zile huduma  na kuwafikia wananchi zaidi kwenye maeneo hayo,”alisema Dkt Malima.  

Naye Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dkt. Laria Koko, amesema maboresho ya huduma hizo yatachangia wagonjwa kufika kwa wakati katika vituo vya afya na hivyo kupunguza madhara yanayotokana na ucheleweshaji wa huduma muhimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, amepongeza chama hicho kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya sekta ya afya na kwa kujitoa kwao kuwahudumia Watanzania kwa weledi na moyo wa kizalendo.

Maboresho ya miundombinu, upatikanaji wa vifaa vya kisasa, na usambazaji wa huduma hizi hadi ngazi ya wilaya si tu yatapunguza mzigo kwa hospitali za rufaa, bali pia yataokoa maisha ya Watanzania wengi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com