Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AJENDA YA NISHATI SAFI YAPATA NGUVU MPYA KWA UZINDUZI WA MKAKATI WA MAWASILIANO


Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Zaidi ya watu bilioni 2.1 duniani ambao ni sawa na asilimia 24.7 ya wakazi wote wa dunia hawana huduma ya nishati safi ya kupikia, huku milioni 990 kati yao wakitokea Afrika.

Katika kundi hilo, wanawake na watoto wenye umri chini ya miaka mitano ndio waathirika wakuu kutokana na athari za kiafya zitokanazo na matumizi ya nishati chafu.

Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Tanzania imezindua Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uelimishaji, ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameeleza hayo wakati akizindua mkakati huo jijini Dodoma, Juni 2, 2025, na kusisitiza kuwa mkakati huo hautakiwi kubaki kama nyaraka tu katika makabati, bali utekelezwe kikamilifu kuanzia ngazi ya mtaa hadi Taifa zima.

“Lazima mkakati huu utekelezwe kwa vitendo. Hatutaki tuwe na nyaraka nzuri zisizofanyiwa kazi. Kila mmoja wetu anayo nafasi ya kuchangia katika mapinduzi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kueleza kuwa tangu kuzinduliwa kwa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Mei 8, 2024, matumizi ya nishati hiyo yamepanda kutoka asilimia 6 hadi 16 ndani ya kipindi kifupi.

Serikali pia imeanzisha Kitengo Maalum cha Nishati Safi ya Kupikia kwa ajili ya kuratibu miradi, kampeni na shughuli zote za kitaifa zinazolenga kuimarisha matumizi ya nishati hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa kwa mafanikio.

Dkt. Biteko amesisitiza kuwa kila taasisi inapaswa kutambua nafasi yake katika kuendeleza matumizi ya nishati salama huku akitoa wito kwa vyombo vya habari, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kushirikiana kikamilifu kwenye kampeni, ikiwa ni pamoja na kuweka mkazo kwa makundi maalum ya jamii.

Ametaja kampeni nyingine kuwa ni Kuelimisha kuhusu njia nafuu za ufadhili

na kuhakikisha ujumbe thabiti unafika kwa walengwa wote.

Katika kuhakikisha utekelezaji wa mkakati huo unakwenda sambamba na malengo yaliyopangwa, ameagiza Kitengo cha Tathmini na Ufuatiliaji cha Wizara ya Nishati kufanya tathmini ya kila robo mwaka ili kutathmini maendeleo na kuchukua hatua mapema endapo kutakuwa na changamoto.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameeleza kuwa Mkoa wake umechukua hatua za makusudi kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ambapo magereza tisa, shule tisa za bweni na VETA tatu tayari zinatumia nishati hiyo.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema kuwa sekta ya nishati imepiga hatua kubwa katika miaka minne iliyopita, huku nguvu ya ushawishi ya Rais Samia ikichangia kwa kiasi kikubwa kupokewa kwa ajenda ya nishati safi ndani na nje ya nchi.

“Mkakati huu wa mawasiliano utasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa programu mbalimbali na kusaidia Watanzania wengi zaidi kuhama kutoka matumizi ya nishati chafu,” amesema Kapinga.

Nao wadau Nishati wa kimataifa akiwemo Mratibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema mkakati huo umeandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), ukiongozwa na kaulimbiu ya kitaifa: “Nishati Safi ya Kupikia, Okoa Maisha na Mazingira.”

Kwa upande wake, Rodney Thadeus kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ameahidi ushirikiano wa karibu kuhakikisha ujumbe kuhusu nishati safi unawafikia wananchi kupitia vyombo vya habari.

Mshauri wa Rais anayeshughulikia Nishati Safi ya Kupikia na Maendeleo ya Jamii, Bi. Angellah Kairuki, alisema kuwa uzinduzi wa mkakati huo ni ushahidi wa jinsi Serikali inavyotoa kipaumbele katika kulinda afya za wananchi na mazingira.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com