Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AFYA YA MTUMISHI, NGUZO YA MAGEUZI KATIKA SEKTA YA MADINI – MAVUNDE




Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameongoza bonanza la michezo lililolenga kuimarisha afya, mshikamano na morali ya kazi kwa watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake, akibainisha kuwa ustawi wa mtumishi ni nguzo ya msingi katika kufanikisha mageuzi ya Sekta ya madini.

Akizungumza katika bonanza la michezo lililoandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Taasisi zake Jijini Dodoma Juni 28, 2025, Mavunde amesema kuwa mtumishi wa umma mwenye afya bora, ari na mshikamano na wenzake ndiye chachu ya mabadiliko na ufanisi kazini.

“Tumeamua kuwekeza kwa vitendo kwenye afya na ustawi wa watumishi wetu kwa sababu tunajua kuwa, nyuma ya mafanikio ya kila sera na mradi mkubwa, kuna mtumishi mwenye afya na ari ya kazi, "amesema

Ameongeza kuwa Bonanza hilo si burudani tu bali ni sehemu ya mikakati ya Wizara hiyo katika kujenga Taasisi thabiti

Aidha, ametumia jukwaa hilo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya sera, uongozi na utekelezaji yaliyowezesha mageuzi yanayoonekana kwenye sekta ya madini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, ufanisi katika sekta unahitaji timu yenye afya njema, maadili ya kazi, mshikamano na ubunifu ambavyo vyote kwa pamoja ni misingi iliyowekwa kupitia bonanza hilo la michezo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Yahya Ismail Samamba ameeleza kuwa bonanza hilo si tukio la kawaida bali ni utekelezaji wa sera ya maendeleo ya rasilimali watu kwa njia ya afya, ustawi na mshikamano kazini.

“Tumejifunza kwamba afya bora inakwenda sambamba na tija kazini, Michezo kama hii hutoa nafasi ya kutathmini sio tu hali ya miili yetu, bali pia mahusiano na hali ya mazingira ya kazi tunayoshiriki kila siku,” amesema Katibu Mkuu.

Ameongeza kuwa mabonanza hayo yamekuwa sehemu ya kalenda ya wizara, na kwamba michezo si burudani pekee bali ni fursa ya kujifunza, kuunganishwa na kujipanga upya kwa mafanikio makubwa zaidi.

Naye Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, ametumia nafasi hiyo kumpa heshima Waziri kwa kuwa kiongozi anayeamini katika ushirikiano, uthubutu na ufuatiliaji wa karibu sifa ambazo, amesema, zimepelekea mafanikio yanayoonekana katika sekta hiyo.

Ametaja Maono ya Bonanza hilo kuwa ni Kuimarisha afya na kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza,kuweka msingi wa ushirikiano na mshikamano kazini,Kukuza ari ya utumishi, uwajibikaji na kuhimiza morali ya kazi na kutekeleza kwa vitendo miongozo ya Serikali kuhusu afya kazini ikiwa ni pamoja na kujenga taswira chanya ya sekta ya madini kama chombo cha maendeleo ya kweli.

Katika tukio hilo, michezo mbalimbali ilishirikisha watumishi kutoka Wizara ya Madini, STAMICO ,GST, na Taasisi nyingine, hali iliyojenga ari ya pamoja na kuonesha kuwa maendeleo ya sekta hayawezi kutenganishwa na ustawi wa rasilimali watu.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com